NEWSPOINTTZ.BLOGSPOT.COM

Usajili wa asasi,vyama, misikiti na vikundi wasitishwa

 
WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe ameuagiza Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kusitisha mara moja usajili mpya wa wadhamini wa asasi, vyama, misikiti na vikundi mbalimbali vya kijamii kwa lengo la kufanya uhakiki wa uhalali wa kuwepo wa taasisi hizo kisheria.

Ameagiza kuwa uhakiki huo ukamilike ndani ya miezi mitatu (siku 90) kuanzia sasa na orodha kamili ya wadhamini ikiwa ni pamoja na picha zao, anuani ya posta na makazi, na taarifa nyingine muhimu za utambuzi wa taasisi hizo mahali zilipo. 

Taarifa hizo ziwasilishwe Rita na nakala wizarani kwa uhakiki na kumbukumbu.

Dk Mwakyembe alitoa agizo hilo, alipokutana na watendaji na uongozi wa Bodi ya Rita, Dar es Salaam jana kwa lengo la kuboresha utendaji wa Wakala na kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano. Rita ina zaidi ya wadhamini 5,000 walio kwenye vitabu vyao vya usajili.

Aidha, Waziri huyo ameitisha kikao wiki ijayo cha mamlaka zote zinazohusika na usajili wa vikundi vya kijamii, mashirika, kampuni na asasi mbalimbali kwa lengo la kuimarisha taratibu za usajili na uendeshaji na kuboresha mawasiliano baina ya vyombo vya usajili vya dola ili kulinda maslahi mapana ya Taifa.
Share on Google Plus

News Point inakusogezea habari kubwa za kila siku kutoka kila kona ya dunia. Ungana nasi kupitia Facebook , Twitter na Instagaram ili uwe wa kwanza kupata habari.

0 comments:

Post a Comment