Mfalme
wa Saudi Arabia Mtukufu Salman Bin Abdulaziz Al Saud amemhakikishia
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, kuwa
nchi yake imeichagua Tanzania kuwa nchi ya kipaumbele katika mpango wake
wa kuimarisha zaidi mahusiano na Afrika uliolenga kuendeleza na kukuza
biashara, uwekezaji na kushiriki katika miradi ya maendeleo.
Ujumbe
wa Mtukufu Salman Bin Abdulaziz Al Saud umewasilishwa kwa Rais Magufuli
jana tarehe 24 Machi, 2016 na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia
Mheshimiwa Adel Al Jubeir Ikulu Jijini Dar es salaam.
Katika
Salamu hizo pamoja na kumpongeza Rais Magufuli kwa kuchaguliwa
kuiongoza Serikali ya awamu ya tano ya Tanzania, Mfalme Salman Bin
Abdulaziz Al Saud amesema Saudia Arabia imedhamiria kukuza zaidi
mahusiano kati yake na Tanzania ili kuwaletea manufaa makubwa wananchi.
Kwa
upande wake Rais Dkt. John Pombe Magufuli amemshukuru Mfalme wa Saudi
Arabia kwa kumtumia ujumbe na kumpongeza kwa kuchaguliwa kuiongoza
Tanzania na amemhakikishia kuwa Serikali yake itafurahi kuona Saudi
Arabia inashirikiana na Tanzania kutekeleza miradi mikubwa ikiwemo
ujenzi wa Reli ya Kati na barabara.
Maeneo
mengine ambayo Rais Magufuli na Waziri Adel Al Jubeir wameyazungumzia
ni ushiriakiano kati ya Tanzania na Saudia Arabia katika kuendeleza
Elimu, Utalii, Bandari na miundombinu.
Pamoja
na kufanya Mazungumzo hayo, Rais Magufuli pia ameshuhudia utiaji saini
wa mkataba kuhusu ushirikiano kati ya Tanzania na Saudi Arabia katika
nyanja za Uchumi, Biashara, Uwekezaji, Ufundi, Vijana na Michezo, ambapo
kwa upande wa Tanzania mkataba huo umesainiwa na Waziri wa Mambo ya
Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Balozi
Augustine Mahiga, na kwa upande wa Saudi Arabia umesainiwa na Waziri wa
Mambo ya Nje wa Saudi Arabia Mheshimiwa Adel Al Jubeir.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
24 Machi, 2016
0 comments:
Post a Comment