NEWSPOINTTZ.BLOGSPOT.COM

Halima Mdee Amtaka Rais Magufuli Ataje Posho na Marupurupu Anayolipwa



Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Halima Mdee amemuomba Rais John Magufuli kuweka wazi posho na marupurupu anayoyapata ili Watanzania wajue kiasi halisi anachokipata mbali na mshahara wake.

Mdee ambaye ni mbunge wa Kawe, alitoa ombi hilo jana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya Sokoni, Jimbo la Mtama mkoani Lindi, uliohudhuriwa na mamia ya wananchi wa jimbo hilo.

Kauli hiyo ya Mdee imekuja siku moja baada ya Rais Magufuli kutaja mshahara wake kuwa ni Sh9.5 milioni kwa mwezi. 

“Juzi Rais anasema eti mshahara wake Sh9.5 milioni, sasa atutajie posho za kila siku ili kila Mtanzania ajue kiasi ambacho anakipata,” alisema Mdee.

Mdee aliongeza kuwa wabunge wanalipwa mshahara wa Sh3 milioni, lakini kuna posho mbalimbali kutokana na kuhudumia wananchi.

“Sisi wabunge mshahara wetu katika hati ya mshahara unasomeka Sh3 milioni, lakini posho na pesa ya mambo ya utendaji ya mbunge inafika Sh10 milioni, Rais atuambie na yeye posho zake ni kiasi gani,” alisema Mdee.

Mbunge wa Jimbo la Ndanda katika Wilaya ya Masasi, Cecil Mwambe alidai katika mkutano huo kuwa wananchi wa Mtama wamekosa mwakilishi wa kuwasemea matatizo yao, hasa ya upande wa kilimo cha korosho kutokana na mbunge wao, Nape Nnauye kukosa uwezo wa kusimama bungeni kuisema Serikali.

“Mtama mmekosa mwakilishi, hapa kuna tatizo la korosho na mbunge aliyepo anashindwa kulisemea, hivyo mtabaki hivyo hivyo bila kutatua tatizo lenu kwa kipindi cha miaka mitano,” alidai Mwambe.
Share on Google Plus

News Point inakusogezea habari kubwa za kila siku kutoka kila kona ya dunia. Ungana nasi kupitia Facebook , Twitter na Instagaram ili uwe wa kwanza kupata habari.

0 comments:

Post a Comment