Polisi
mkoani Morogoro inamshikilia Juma George (29) mkazi wa Shinyanga, kwa
kukutwa na silaha ya kivita aina ya SMG iliyofutwa namba zake za
usajili, magazini mbili, risasi 21 pamoja na panga vikiwa vimehifadhiwa
ndani ya begi lake la nguo.
Kamanda
wa Polisi wa mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei, alisema mtuhumiwa huyo
ambaye ni dereva alikamatwa Machi 30, mwaka huu saa mbili usiku maeneo
ya stendi kuu ya mabasi ya Msamvu, mjini Morogoro.
Kamanda
Matei alisema, askari wakiwa doria katika eneo hilo walipata taarifa
kutoka kwa raia mwema kuwa kwenye basi lenye namba za usajili T.141 DEE
aina ya Yutong mali ya Kampuni ya Nyahunge likitokea Shinyanga kwenda
Morogoro kuna abiria mmoja amehifadhi silaha.
Alisema
baada ya askari kupata taarifa walifika eneo la stendi ya Msamvu na
walifanikiwa kumkamata mtu huyo. Ilielezwa kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa
akitokea mkoani Shinyanga akielekea Tarafa ya Mngeta, wilaya ya
Kilombero.
Kamanda
wa Polisi Matei alisema, uchunguzi bado unaendelea na utakapokamilika
mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu shitaka linalomkabili.
Katika
tukio jingine, Ester Abel (43) mkazi wa Mbumi B Tarafa ya Kilosa,
wilayani Kilosa, mkoani Morogoro anashikiliwa na Polisi kwa kukutwa na
dawa za kulevya zinazodhaniwa kuwa ni kokeni kete 780 , kilogramu mbili
za bangi na misokoto 25 iliyohifadhiwa kwenye mfuko wa nailoni.
Kamanda
wa Polisi wa mkoa wa Morogoro, Matei alisema kuwa mwanamke huyo
alikamatwa Machi 30, mwaka huu saa 2:15 usiku katika eneo la Mbumi B ,
tarafa ya Kilosa Mjini, wilayani humo, mkoani Morogoro .
Kamanda
wa Polisi Matei alisema, inadaiwa kuwa mtuhumiwa huyo ni muuzaji wa
dawa za kulevya na kwamba uchunguzi unaendelea na atafikishwa mahakamani
mara moja baada ya kukamilika kwake.
chanzo>mpekuzi
0 comments:
Post a Comment