NEWSPOINTTZ.BLOGSPOT.COM

Hatima ya Mkataba Tata wa Lugumi Mikononi mwa Spika Job Nduagai


Hatima ya mkataba tata wa kampuni ya Lugumi Enterprises ipo mikononi mwa Spika wa Bunge, Job Ndugai baada ya jana, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuwasilisha muhtasari wa ilichokibaini baada ya kupitia maelezo ya utekelezaji wake.

Moja kati ya mambo yaliyomo katika muhtasari huo ni kulitaka Bunge kutoa ruhusa kwa kamati ndogo iliyoundwa na PAC juzi kuchunguza kwa kina mkataba huo wa kufunga mtambo wa utambuzi wa vidole (AFIS), ikiwa ni pamoja na kutembelea vituo vinavyodaiwa kufungwa mashine hizo.

Kamati ya PAC ilinusa ufisadi kwenye mkataba huo wa AFIS ulioitaka Lugumi kufunga mitambo kwenye vituo vya polisi 108 kwa gharama ya Sh37 bilioni lakini ilibainika kwamba kampuni hiyo ililipwa kiasi cha Sh34 bilioni zaidi ya asilimia 90 ya fedha zote ilhali imefunga mashine 14 tu mkoani Dar es Salaam.

Makamu Mwenyekiti wa PAC, Aeshi Hilaly alisema jana muda mfupi baada ya kukutana na Spika kuwa wamepeleka mapendekezo hayo na wanachokisubiri ni kauli ya ofisi yake.

Muhtasari huo umekuja siku moja baada ya PAC kuwaweka kitimoto Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Projest Rwegasira na Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Abdulrahman Kaniki kuhusu mkataba huo. 

Bunge liliagiza maelezo ya kina kwa maandishi kuhusu utekelezaji wa mradi huo baada ya kubaini kuwa una maswali mengi kuliko majibu na liliwaita viongozi hao ili kupata ufafanuzi wa kina.

Katika maelezo yake jana, Aeshi alisema kesho watakuwa wameshapata majibu kutoka Ofisi ya Spika na wataweka wazi mambo yote waliyokuwa wakiyajadili kuhusu Lugumi.

“Hili ni jambo zito ambalo linahusu usalama kwa hiyo ni lazima twende nalo taratibu ili kujua ukweli na kuja na majibu ya kueleweka... kila kitu tutawaeleza Jumamosi,” alisema.
Share on Google Plus

News Point inakusogezea habari kubwa za kila siku kutoka kila kona ya dunia. Ungana nasi kupitia Facebook , Twitter na Instagaram ili uwe wa kwanza kupata habari.

0 comments:

Post a Comment