Makamu Mwenyekiti wa PAC, Aeshi Hilaly
Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) haijaridhishwa na majibu
yaliyotolewa na maofisa wa juu wa Jeshi la Polisi kuhusu Mkataba wa
Lugumi Enterprises, na hivyo kamati hiyo imeamua kuunda kamati ndogo leo
itakayochunguza kwa undani sakata hilo ambapo ripoti ya uchunguzi
huo itawasilishwa bungeni kama ilivyokuwa sakata la Escrow.
Kwa
mujibu wa taarifa tulizozipata kutoka chanzo cha kuaminika, PAC
haikuridhishwa na majibu ya hoja nyingi zilizotolewa na watendaji wakuu
akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuhusu mkataba
wa Lugumi baada ya kukutana nao jana mjini Dodoma.
“PAC
imelazimika kuunda kamati ndogo kesho (leo), itakayokuwa na nguvu
kuhoji mambo yote ukiwemo mkataba huo kwa sababu majibu yaliyotolewa
hayakuridhisha,” kilieleza chanzo hicho.
Kiliongeza
kuwa baadhi ya mambo yanayokanganya PAC ni kufahamu nani mkweli kati ya
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kupitia taarifa ya
ukaguzi na maelezo ya Jeshi la Polisi kuhusu gharama za mkataba.
Kwa
mujibu wa chanzo chetu, taarifa ya CAG inaonesha kuwa mkataba huo ni wa
Sh bilioni 37.742 wakati maelezo yaliyotolewa na viongozi wa Jeshi hilo
walipohojiwa na PAC hiyo jana, walisema ni Sh bilioni 37.163.
Hivyo
kuwepo kwa tofauti ya zaidi ya Sh milioni 578.972. Aidha, utata
mwingine ni jeshi hilo kukosa maelezo ya kwa nini katika kutafuta
mzabuni kwenye mradi huo, walitumia mfumo wa mzabuni mmoja badala ya
wengi.
Chanzo
chetu kilisema katika mahojiano na viongozi hao wa polisi, walishindwa
kutoa maelezo yanayojitosheleza kwa nini kitengo cha manunuzi cha jeshi
hilo walitumia mfumo huo.
Hivyo kutokana na utata huo, Kamati hiyo imeamua kukutana na Spika leo ili kumtaarifu hatua waliyofikia ya kuunda Kamati Ndogo.
Juzi,
taarifa ya Utekelezaji wa Mkataba tata wa Kampuni ya Lugumi Enterprises
ulioshinda zabuni mwaka 2011 ya kufunga mashine za kuchukua alama za
vidole katika vituo vya polisi vya wilaya nchi nzima kwa gharama ya Sh
bilioni 37, ulitua ndani ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC) na kuanza kujadiliwa.
Akizungumza
juzi bungeni, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Aeshi Hilaly alisema
taarifa ya utekelezaji wa mkataba huo ilifikishwa bungeni Jumatatu na
juzi asubuhi wamepewa na wakaanza kuujadili.
Awali,
Aprili 5, mwaka huu mjini Dar es Salaam, Kamati hiyo ilitoa siku saba
kuanzia siku hiyo kwa Jeshi la Polisi nchini kupeleka mkataba walioingia
baina yao na Kampuni ya Lugumi iliyopewa zabuni ya kufunga mashine 108
katika vituo tajwa nchini ila hadi sasa ni vituo 14 tu ndivyo
vilivyofungwa mashine hizo.
Hatua
hiyo ilikuja baada ya kamati hiyo kukutana na Jeshi hilo kupitia
taarifa ya hesabu za jeshi hilo za mwaka 2013/14 zilizokaguliwa na
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kubainika kuwa
na ukiukwaji wa utekelezaji wa mkataba huo.
Ukiukwaji
wa utekelezaji wa mkataba huo mwingine ni pamoja na kampuni hiyo
kulipwa asilimia 99 ya fedha zote za mkataba huo wenye thamani ya Sh
bilioni 37, huku kazi iliyofanywa ni chini ya robo.
0 comments:
Post a Comment