Ndugu zangu Waandishi wa Habari,
Ndugu Waalikwa,
Naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutujaalia uhai na uzima tukaweza kukutana hapa leo.
Namshukuru
Mwenyezi Mungu pia kwa kuijaalia nchi yetu kwa kiasi kikubwa kubaki
katika hali ya amani na utulivu licha ya jitihada kubwa zilizofanywa na
zinazoendelea kufanywa na baadhi ya watu za kuivuruga amani yetu.
Naendelea
kumuomba Mola wetu aendelee kuibariki nchi yetu na watu wake, aijaalie
kuwa nchi ya amani na atujaalie hekima na busara katika kuendesha mambo
yetu.
Nichukue fursa hii pia kukushukuruni nyinyi waandishi wa
habari kwa kuitikia wito wetu na kuja kutusikiliza. Shukrani maalum zije
kwenu wale ambao mmesafiri kutoka Dar es Salaam na kuja Zanzibar
makhsusi kwa ajili ya mkutano huu.
Tunathamini sana mashirikiano
yenu nyote tukitambua nafasi na mchango mkubwa wa vyombo vya habari
katika maendeleo ya nchi yoyote ile.
Mtakumbuka kwamba siku saba
zilizopita tulizungumza nanyi ambapo tuliwasilisha kwenu maazimio 13 ya
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama Cha Wananchi (CUF) kuhusiana na
msimamo wa Chama chetu dhidi ya ubakaji wa demokrasia Zanzibar
uliofanyika tarehe 20 Machi, 2016 na ambao ulipewa jina la uchaguzi wa
marudio.
Leo hii tumekuiteni ili kutimiza agizo nililopewa na
Baraza Kuu lililonitaka nizungumze na wananchi wa Zanzibar ili kuwaeleza
kwa kina mwelekeo wa hali ya kisiasa ya Zanzibar na hatua
zinazochukuliwa na CUF kuhakikisha maamuzi halali ya kidemokrasia ya
Wazanzibari waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba, 2015 yanaheshimiwa.
UCHAFUZI WA TAREHE 20 MACHI, 2016
Nilieleza
kwa urefu katika mkutano wangu na waandishi wa habari wa tarehe 11
Januari, 2016 nilioufanya Dar es Salaam juu ya nini kilitokea baina ya
tarehe 25 Oktoba 2015 hadi tarehe 28 Oktoba, 2015, siku ambayo
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salim Jecha, alitoa
tangazo batili na haramu la kufuta uchaguzi huru na wa haki uliofanyika
tarehe 25 Oktoba, 2015. Nilieleza pia hoja za kikatiba na kisheria za
kwa nini tangazo lile ni haramu na batili na hoja zile hadi leo watawala
wameshindwa kuzijibu.
Kwa hoja hizo hizo, nikaeleza kwamba
hakuna vifungu vya Katiba wala Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Nam. 11 ya
1984 vinavyozungumzia kitu kinachoitwa uchaguzi wa marudio ukiondoa
pale inapotokea wagombea wanapopata idadi sawa ya kura.
Sikusudii kurudia yale ambayo nilishayaeleza siku ile maana hayo sasa yanaeleweka na kila mtu ndani na nje ya nchi.
Leo
hii nataka niwapongeze kwa mara nyengine tena wananchi jasiri na
shupavu wa Zanzibar kwa kuitumia tarehe 20 Machi, 2016 kukifedhehesha
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa mara ya pili ndani ya miezi sita mbele ya
macho ya Watanzania na mbele ya macho ya jumuiya ya kimataifa.
Wananchi
wazalendo wa Zanzibar wanaoipenda nchi yao waliwakataa watawala waovu
wa CCM na sera zao mbovu zinazoidhalilisha Zanzibar yao kupitia sanduku
la kura tarehe 25 Oktoba, 2015.
Watawala waovu wa CCM wakaamua
kutumia mabavu na uvunjwaji wa katiba na sheria kuyapindua maamuzi ya
Wazanzibari, kwa sababu tu maamuzi hayo yalikuwa ni ya kuwakataa
watawala hao.
Kwa miezi mitano kuanzia Oktoba 2015 hadi Machi
2016, watawala waovu wa CCM wakawaingiza wananchi watulivu na wanaopenda
amani wa Zanzibar katika idhilali na hilaki kubwa kwa kuwazuilia haki
zao za msingi za binadamu ili wasiweze kuonesha hisia zao dhidi ya
watawala.
Kwa namna ya pekee na ya ustaraabu wa hali ya juu na wa
kupigiwa mfano, wananchi wa Zanzibar wakaisubiri tarehe 20 Machi, 2016
na wakapeleka ujumbe wao kwa watawala hao na kwa dunia nzima kwa njia za
amani za kuususia uchafuzi ulioitishwa siku hiyo.
Hali halisi
iliyoonekana na kila aliyetaka kuona ni kwamba zaidi ya asilimia 80 ya
Wazanzibari hawakwenda kupiga kura siku hiyo ili kuonesha hisia zao na
kuthibitisha tena maamuzi yao ya tarehe 25 Oktoba, 2015.
Kituo
cha televisheni cha ITV kilichokuwa kikirusha matangazo ya moja kwa moja
kutoka katika mikoa mitano ya Unguja na Pemba kilionesha vile
vilivyoitwa vituo vya kupigia kura vikiwa havina watu kabisa au vikiwa
na watu wachache sana.
Walipowahoji wale walioitwa maofisa
uchaguzi na walioitwa mawakala kila mmoja alikuwa akija na majibu yake
na takwimu zake zinazopingana na za mwenzake.
Vituo vya
televisheni vya kimataifa hasa kile cha Al-Jazeera na CCTV ya China
vilionesha na kuripoti vituo vikiwa vitupu. Hata televisheni ya watawala
ya ZBC ilikuwa ikipata kigugumizi kuonesha hali ilivyokuwa katika vile
vilivyoitwa vituo vya kupigia kura hadi kuamua kukatisha matangazo ya
moja kwa moja. Magazeti ya Tanzania na ya nje ya nchi yaliripoti na
kuchapisha picha zilizoonesha kususiwa kwa uchafuzi huo ulioitishwa na
watawala wakidhani wanajihalalishia haramu yao.
Mitandao ya
kijamii nayo ilijaa maelezo na vielelezo kutoka watu na taasisi za
kimataifa zinazoheshimika vikionesha hali halisi ilivyokuwa na ujasiri
wa Wazanzibari wa kuususia uchafuzi huo.
Na hatimaye nchi 16
zikatoa taarifa yao tarehe 21 Machi, 2016 wakieleza kwamba uchaguzi huo
haukuwa wa kuheshimika kwa sababu haukuwa shirikishi na wala
haukuwakilisha matakwa ya wapiga kura wa Zanzibar.
Nitumie fursa
hii kwa mara nyengine tena kuwapongeza wananchi wote wa Zanzibar kwa
ujasiri, uzalendo na ari kubwa walioionesha kwa kuitikia kwa kiasi
kikubwa wito wa chama chao cha CUF wa kuwataka wasishiriki katika uhuni
na ubakaji wa demokrasia uliopewa jina la uchaguzi wa marudio wa tarehe
20 Machi, 2016, na hivyo kuudhihirishia ulimwengu kwamba Chama Cha
Mapinduzi (CCM) hakina ridhaa ya wananchi wa Zanzibar.
Naungana
na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF kuwapongeza waliokuwa wagombea
wenzangu wa CUF kwa nafasi za Uwakilishi na Udiwani kwa kusimama na
wananchi wa Zanzibar na kutoshiriki katika uchaguzi huo haramu na batili
wa marudio, jambo ambalo limethibitisha kwamba hawapo kwa ajili ya
kutaka nafasi na vyeo binafsi bali wanachotaka ni kuleta mabadiliko ya
kweli kwa maslahi ya watu wote wa Zanzibar.
Pongezi zangu za
dhati kabisa zinakwenda kwa wagombea Urais, Uwakilishi na Udiwani wa
vyama vyengine vya upinzani ambavyo ni NRA, DEMOKRASIA MAKINI, SAU, UMD,
JAHAZI ASILIA, CHAUMMA, UPDP, DP, na ACT-WAZALENDO, na vile
vinavyoshirikiana kupitia UKAWA ambavyo ni CHADEMA, NCCR na NLD kwa
kuungana pamoja na Wazanzibari kutetea demokrasia yao.
CCM WANAPENDA NAMBA LAKINI HAWAJUI HESABU
Jambo
moja ambalo CCM wamejifedhehesha wenyewe ni lile la kutangaza kile
walichokiita matokeo ya uchafuzi wao bila ya kuzingatia kwamba takwimu
zina sifa moja, huwa hazisemi uongo.
Vijana wana msemo wao siku
hizi; wanasema CCM wanapenda namba lakini hawajui hesabu. Matokeo ya
tarehe 20 Machi, 2016 waliyoyatangaza ni kwamba eti jumla ya watu
waliopiga kura walikuwa 341,865 na kwamba Dk. Ali Mohamed Shein eti
alipata kura 299,982 sawa na asilimia 91.4.
Takwimu za uchaguzi
mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 zilionesha kwamba jumla ya wananchi
waliojitokeza kupiga kura walikuwa ni 402,354 na Dk. Ali Mohamed Shein
alipata kura 182,011 sawa na asilimia 46.28.
Wakati huo huo kwa
uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzaia, wapiga kura kwa
upande wa Zanzibar walikuwa 417,882 ambapo mgombea wa CCM, Dk. John
Pombe Magufuli alipata kura 194,317 sawa na asilimia 46.5.
Kwa
hivyo, kwa kutumia takwimu hizi, mtu anapochukua takwimu hizi na
kulinganisha wapiga kura 402,354 waliojitokeza tarehe 25 Oktoba, 2015 na
wale wanaodai eti walijitokeza tarehe 20 Machi kwamba ni 341,865
watawala wa CCM walichotaka kutuaminisha ni kwamba tofauti ya waliokuwa
hawakujitokeza kupiga kura ilikuwa ni 60,489 tu. Suala la kujiuliza ni
kwamba iwapo hilo ni kweli kwa nini vituo vionekane vitupu kabisa tarehe
20 Machi, 2016?
Lakini kwa upande mwengine, mtu anapokosa hata
tahayuri na kudai Dk. Ali Mohamed Shein amepata kura 299,982 anachotaka
kutwambia ni kwamba ndani ya miezi mitano ya idhilali na mateso
aliyowapatisha Wazanzibari ameweza kuongeza kura 117,971.
Kufedheheka
kwa CCM kunakuja zaidi kwamba walisahau kwamba waliyakubali matokeo ya
uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa tarehe 25 Oktoba 2015 kwa
upande wa Zanzibar ambapo kama tulivyokwisha onesha waliopiga kura
walikuwa wengi zaidi wakiwa ni 417,882 (na hilo ungetegemea
lingeinufaisha CCM) na bado mgombea wa CCM akapata kura 194,317 sawa na
asilimia 46.5. Kwa kutumia idadi waliyotangaza ya kura 299,982 walizompa
Dk. Shein wanataka kutwambia kwamba yeye amepata kura 105,665 zaidi
kuliko Dr. Magufuli kwa Zanzibar.
Kama takwimu zao zingekuwa
sahihi ina maana pia wapiga kura waliomuunga mkono mgombea wa CUF ambao
hawakwenda kupiga kura ni 60,489 tu (sawa na asilimia 15 tu). Hivi nani
utamdanganya kwamba Maalim Seif Sharif Hamad anaungwa mkono na asilimia
15 tu ya wapiga kura wa Zanzibar? Nani utamdanganya kwamba ndani ya
miezi mitano, CCM imeongeza kura 105,665 zaidi ya alizopata mgombea wake
Dk. Magufuli kwa upande wa Zanzibar?
Kutokana na ubabe na kiburi
cha utawala walicho nacho CCM, wameishia kujifedhehesha kwa takwimu zao
za kupika wenyewe. Ndiyo vijana wakasema, CCM wanapenda namba lakini
hawajui hesabu.
NINI MWELEKEO WA CUF NA WAZANZIBARI BAADA YA UBAKAJI HUU WA DEMOKRASIA?
Wazanzibari
walio wengi wamekuwa wakituuliza nini mwelekeo wa CUF baada ya ubakaji
huu wa demokrasia? Wanatuuliza viongozi wao na hasa mimi tunatokaje
katika hali hii ambayo imedumu miaka nenda miaka rudi kila pale Zanzibar
inapofanya uchaguzi?
Kabla sijalieleza hilo, nataka niweke wazi
leo kwamba tulipofanya uamuzi wa kuususia uchaguzi haramu na batili wa
tarehe 20 Machi, 2016 tuliamua kusimama juu ya uamuzi unaoheshimu
misingi ya kikatiba ambayo watu wa Zanzibar tumeamua ndiyo inapaswa
iongoze na iendeshe nchi yetu. Tulijua kwamba uamuzi huo utakuwa na
athari kwa CUF na kwa Zanzibar lakini tulijua na tuliamini pia kwamba
athari hiyo haiwezi kuwa kubwa zaidi kuliko gharama ya kuikanyaga Katiba
na Sheria za nchi yetu na gharama za kupiga teke demokrasia, haki za
binadamu na utawala wa sheria.
Tulipima na tukatafakari kwa kina
na kuona ni kheri kumeza machungu ya athari binafsi kwetu lakini
tusimame kidete na kifua mbele katika kutetea maamuzi ya watu wa
Zanzibar waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba, 2015, na pia kulinda misingi ya
Katiba na Sheria za nchi yetu na misingi ya demokrasia na haki za watu.
Tuliona hayo ni kheri kwa huko twendako badala ya kushiriki katika
haramu ya ubakaji wa demokrasia na matumizi ya nguvu za kijeshi
kulazimisha watawala wasio na ridhaa ya watu.
Tulifanya maamuzi
yale pia kwa lengo la kuepusha shari katika nchi yetu. Leo Wazanzibari
na dunia nzima ni mashahidi kwamba uamuzi ule ulikuwa sahihi na wa
busara. Maana mateso na vitisho walivyokumbana navyo Wazanzibari wakati
tumewaachia uchaguzi ule watawala waovu peke yao vilikuwa vya kiasi kile
kilichoshuhudiwa.
Je, tungeliamua kushiriki na kusimama kulinda
na kutetea ushindi wetu hali ingekuwaje? Bila shaka nchi ingetumbukia
katika machafuko ambayo watawala waovu walikuwa tayari yatokee kuliko
kuridhia maamuzi halali ya wananchi wa Zanzibar.
Maamuzi yale
yamethibitika pia kwamba ni sahihi kwa jinsi watu wa Zanzibar
walivyoudharau na kuupuuza uchaguzi haramu na batili wa tarehe 20 Machi,
2016. Watawala waovu wa CCM waliwadharau watu wa Zanzibar na watu wa
Zanzibar wakaamua kuwadharau wao tarehe 20 Machi 2016.
Kwa upande
mwengine, uamuzi tuliouchukua na kuusimamia pia ni uamuzi uliosimama
juu ya misingi ya heshima na misingi ya utu wa watu, ambayo yalikuwa
ndiyo malengo sahihi ya Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar,
Hayati Mzee Abeid Amani Karume, malengo sahihi ya Chama cha Afro Shirazi
na malengo sahihi ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964.
Kwa hakika,
uamuzi wa kuupuuza na kuudharau uchafuzi wa tarehe 20 Machi, 2016 ni
ushindi mwengine wa Zanzibar katika historia yake ya kisiasa.
Nimalizie
sasa kwa kujibu hoja ya ni upi mwelekeo wa CUF na wa Wazanzibari baada
ya ubakaji huu wa wazi wa demokrasia na haki za watu wa Zanzibar?
Kwanza,
nirudie na kusisitiza msimamo wetu kwamba hatukubaliani na ubakaji wa
demokrasia na haki za watu wa Zanzibar uliofanywa na watawala waovu
wakisaidiwa na vyombo vya dola. Kwa msingi huo, Wazanzibari wataendelea
kuipinga serikali isiyo na ridhaa ya watu kwa kutumia njia za amani, za
kidemokrsia na zinazoendana na misingi ya Katiba na Sheria za nchi yetu.
Jana
kumetangazwa kile kilichoitwa ni Baraza la Mawaziri. Msimamo wetu uko
pale pale. Kama tusivyomtambua aliyelitangaza Baraza hilo, vivyo hivyo
hatulitambui Baraza lake la Mawaziri.
Kwa hakika, kwa sababu
msingi wa watawala waliojinyakulia madaraka ni kupitia uvunjwaji wa
Katiba, kila kinachofuata kimekuwa kikiendeleza uvunjwaji wa Katiba.
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kupitia Marekebisho ya 10 ya mwaka
2010, Ibara ya 9 (1) inalazimisha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa
na muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Ibara za 39, 39A na
42 za Katiba zimeeleza namna Serikali hiyo ya Umoja wa Kitaifa
itakavyoundwa. Masharti yote hayo yanaendelea kuvunjwa na mtawala
aliyeamua kuyapiga teke maamuzi ya Wazanzibari na kujiweka madarakani
kwa nguvu. Kwa hivyo, Serikali yake haiwezi kuwa Serikali inayokwenda na
Katiba. Kwa ufupi, si Serikali halali kwa mujibu wa Katiba.
Baraza
Kuu la Uongozi la Taifa la CUF katika kikao chake cha tarehe 2 – 3
Aprili, 2016 lilipitisha maazimio yafuatayo miongoni mwa maazimio yake:
“Azimio Nam. 9:
Haliyatambui
matokeo ya uchaguzi huo haramu na batili, na kwa msingi huo halimtambui
Dk. Ali Mohamed Shein kuwa Rais wa Zanzibar, haliwatambui waliotangazwa
kuwa Wawakilishi na wala haliwatambui waliotangazwa kuwa Madiwani.
Baraza Kuu linaungana na wananchi wa Zanzibar waliokataa kuwapa uhalali
watu hao na kwa hivyo halitoitambua Serikali, Manispaa na Halmashauri za
Wilaya zitakazoundwa na watu hao. CUF haitoshirikiana na Serikali
itakayoundwa kwa sababu ni kinyume na Katiba ya Zanzibar, kinyume na
Sheria ya Uchaguzi na haikutokana na ridhaa ya watu. Kwa vyovyote vile,
Serikali itakayoundwa haitakidhi matakwa ya Katiba ya Zanzibar na hivyo
CUF haitoshiriki kwenye uvunjaji wa Katiba ambayo inaeleza kwa uwazi
kabisa namna ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.
“Azimio Nam. 10:
Linawataka
wananchi wote wa Zanzibar kutumia njia za amani, za kikatiba na
kisheria ambazo zimewahi kutumika katika nchi nyingine duniani kuwakataa
watawala waovu na wasio na ridhaa ya watu waliojiweka madarakani kwa
kutumia nguvu na ubakaji wa demokrasia kwa kutoipa ushirikiano Serikali
itakayoundwa na watawala hao.”
Baada ya maazimio hayo ya Baraza
Kuu, kinachofuata sasa ni utekelezaji wake. Hivi sasa tunapanga mikakati
madhubuti ya utekelezaji wa maazimio hayo kwa kutumia njia za amani, za
kidemokrasia na za kikatiba ili kutufikisha kwenye malengo yetu ya
kuona maamuzi ya watu wa Zanzibar yanaheshimiwa.
Nina hakika kabisa
kuwa mikakati tunayoipanga itazaa hatua ambazo zitaibana Serikali haramu
na hatimaye itasalimu amri kwa wananchi wa Zanzibar ambayo kwa mujibu
wa Katiba ya Zanzibar ndiyo wenye mamlaka ya kuiweka madarakani Serikali
wanayoitaka. Katika dunia ya leo, hatuwezi kuongozwa na watawala ambao
hawakupewa mamlaka na watu wenyewe.
Pili, naipongeza na
kuishukuru jumuiya ya kimataifa na washirika wa maendeleo kwa msimamo
waliochukua wa kukataa kubariki ubakaji huo wa demokrasia na haki za
watu wa Zanzibar na kukataa kushiriki katika uapishwaji wa mtu asiye na
ridhaa ya wapiga kura wa Zanzibar. Napongeza hatua ambazo wameanza
kuzichukua dhidi ya Serikali za CCM ambazo ndizo zilizosimamia ubakaji
huo wa demokrasia na haki za watu. Natoa wito kwao kuchukua hatua kali
zaidi dhidi ya watawala hawa waovu zikiwemo kuwawekea vikwazo vya
kusafiri, kufuatilia akaunti zao za fedha nje ya nchi na hatua za
kuchunguza matendo yao ya uhalifu dhidi ya binadamu. Wananchi
waliodhulumiwa haki zao wanaziunga mkono hatua hizo wakiamini kwamba CCM
ni lazima iwajibishwe kwa matendo yake maovu dhidi yao.
Nitumie
fursa hii kwa mara nyengine tena kuwataka wananchi wa Zanzibar kudumisha
amani ya nchi yetu na umoja wa watu wetu. Nikiwa kiongozi wao
ninayewapenda na ambaye nimejitolea kuwatumikia katika umri wangu wote
siwezi kuwaongoza kuelekea kwenye fujo na ghasia au vitendo
vitakavyopelekea kuiharibu nchi yetu na kuathiri watu wetu. Nina imani
kabisa kwamba njia tunayoifuata ni njia ya haki; na haki siku zote
itashinda.
Mwaka 2009, mimi na mwenzangu, Dk. Amani Abeid Karume,
tuliwaongoza Wazanzibari katika Maridhiano yaliyoashiria mwanzo wa
ujenzi wa mahusiano mapya baina ya watu wema wa Zanzibar kwa kuzika
siasa za ubaguzi, utengano, chuki, hasama na fujo na badala yake
kusimamisha siasa za maelewano, umoja, upendo, mshikamano na udugu
katika jamii yetu.
Tulitegemea kuanzia pale tungeendelea mbele
kwa kuchukua hatua za kuyaimarisha maridhiano yetu na kuyazamisha zaidi
kwenye nyoyo za Wazanzibari. Binafsi nasikitishwa na kuhuzunishwa sana
kuona watawala waovu wasiowatakia mema watu wa nchi hii wameturudisha
tulikotoka kwa maslahi yao binafsi.
Natoa wito kwa Wazanzibari
wenzangu kuwa tukatae kurudishwa kwenye siasa zile za ubaguzi, utengano,
chuki, hasama na fujo na kila mmoja afanye lile liliomo katika uwezo
wake kuendeleza maelewano, umoja, upendo, mshikamano na udugu katika
jamii yetu.
Wazanzibari tumeamua kuisimamisha tena Zanzibar yetu
na Zanzibar itasimama tena Inshallah. Hilo sina wasiwasi nalo kama
kiongozi wa Wazanzibari waliyenipa ridhaa yao.
HATIMAYE TUTASHINDA.
WANANCHI JASIRI NA SHUPAVU WA ZANZIBAR WATASHINDA.
Ahsanteni sana.
Home / News
/ HOTUBA YA MAALIM SEIF SHARIF HAMAD KWENYE MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI – PARK HYATT ZANZIBAR, TAREHE 10 APRILI, 2016
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment