Serikali
ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli, itaendelea kupambana na vitendo
vya rushwa na ufisadi kwa nguvu zote bila kutetereka.
Lengo
la hatua hiyo ni kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali na
kuboresha uwajibikaji na maadili katika usimamizi wa rasilimali za umma
na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Makamu
wa Rais, Samia Suluhu Hassan alisema hayo katika hotuba yake kwa Taifa
wakati wa sherehe ya uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru uliofanyika
jana kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Hivyo
aliwaomba Watanzania wote kuunga mkono kwa vitendo juhudi na maelekezo
ya Dk Magufuli za hatua anazozichukua dhidi ya vitendo vya rushwa na
ufisadi nchini.
Kutokana
na hatua hizo, Makamu wa Rais alisema hadi sasa jumla ya kesi 596 za
rushwa zinaendelea mahakamani na jumla ya Sh 6,543,342,793 tayari
zimeokolewa.
“Naomba nitumie fursa hii kuwakumbusha Watanzania wenzangu kujiepusha na vitendo vya kutoa na kupokea rushwa,” alisema
Samia na aliwataka watumishi wa umma, watumishi katika sekta binafsi,
wajasiriamali na kila mmoja kujiepusha na vitendo vya rushwa na
kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia katiba, sheria, kanuni, miongozo
na taratibu zilizowekwa.
“Kama
nilivyokwishasema mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu zinaendelea
kuhimiza mapambano dhidi ya Rushwa chini ya kaulimbiu “Timiza Wajibu
wako, kata Mnyororo wa Rushwa,” aliongeza Makamu wa Rais.
Samia
alisema suala la rushwa limeongelewa mara nyingi na athari zake
zinajulikana ikiwa ni pamoja na ubadhirifu wa mali za umma, mikataba
isiyofaa kwa taifa na udanganyifu na kupokea fedha ili kukiuka sheria
kwa manufaa binafsi huchangia kwa kiwango kikibwa kuwanyima wananchi
hazi zao na kudhoofisha ustawi wa taifa letu.
Mbali
na hatua hiyo ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuendelea na mapambano
dhidi ya rushwa na ufisadi, pia alisisitiza kwa mara nyingine kwa kusema
kuwa Serikali haina nia ya kumwonea mtu inapochukua hatua ya kutumbua
majipu kwa watumishi wa umma.
Akishangiliwa
na wananchi wakati akiwahutubia kwenye sherehe hizo, Makamu wa Rais
alisema lengo la Serikali la kutumbua majipu ni kurekebisha na kurejesha
nidhamu, uadilifu na uwajibikaji serikalini kama ilivyoagizwa katika
Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili Watanzania wote wafaidike na
matunda ya nchi yao.
“Mnasikia
katika Serikali ya Awamu ya Tano tunarekebishana, majipu yanatumbuliwa
...kwa kweli hatuna nia ya kumwonea mtu, tunarekebishana na hilo ndilo
lililomo katika agizo ya Ilani yetu ya CCM ili kuwanufaisha Watanzania
wote wafaidi matunda katika nchi yao,” alisema Makamu wa Rais.
0 comments:
Post a Comment