Ofisi ya Taifa ya Takwimu imetangaza Mfumuko wa Bei wa Taifa wa mwezi Machi
2016 na kusema kuwa umepungua kidogo hadi kufikia asilimia 5.4 kutoka
asilimia 5.6.iliyokuwepo mwezi Februari, 2016.

Hii inamaanisha kuwa  kasi ya upandaji wa bei ya  bidhaa na huduma kwa
mwezi Machi 2016 imepungua kidogo ikilinganishwa na kasi ya upandaji wa bei
ya bidhaa na huduma  iliyokuwepo mwezi Februari mwaka huu.

Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya
Takwimu (NBS) Bw. Ephraim Kwesigabo akitoa taarifa ya Mfumuko wa Bei  wa
Mwezi Machi, 2016 leo jijini Dar es salaam amesema kuwa kupungua kwa
mfumuko huo kumesababishwa na kupungua kwa bei ya bidhaa za vyakula na
bidhaa zisizo za vyakula katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema Takwimu zilizokusanywa katika mikoa yote ya Tanzania Bara Machi
2016 kwa mujibu wa bei za bidhaa zilizoainishwa kupima mfumuko wa bei
zinaonyesha kuwa bidhaa zisizo za vyakula katika soko zikiwemo Gesi, dizeli
na mafuta ya taa zimechangia kupungua kwa mfumuko huo.

Amesema kuwa pamoja na kupungua kwa kasi ya upandaji wa bei ya bidhaa hizo
mwezi Machi mwaka huu baadhi ya bidhaa za vyakula zikiwemo za mchele,
Mahindi, vyakula kwenye Migahawa na mkaa zimeonesha  kuongezeka  katika
soko.

 Kuhusu Fahirisi za Bei ambacho ni kipimo kinachotumika kupima mabadiliko
ya bei ya bidhaa na huduma zinazotumiwa na kaya binafsi hapa Tanzania kwa
mwezi Machi, Kwesigabo amesema kuwa zimeongezeka hadi kufikia 101.93 kutoka
101:44 za mwezi Februari.

Amesema baadhi ya bidhaa za vyakula za vyakula zikiwemo unga wa muhogo,
matunda, maharagwe na samaki zimechangia kuongezeka kwa Fahirisi hizo na
kuongeza kuwa bidhaa zisizo za vyakula zilizochangia ongezeko hilo ni
Mavazi ya wanawake, mkaa na kuni.

Kwa upande wa uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na
huduma za mlaji kwa mwezi Machi , 2016 umefikia shilingi 98 na senti 11
ikilinganishwa na uwezo wa shilingi 98 na senti 58  wa mwezi Februari 2016.

“Uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma zilezile
kwa mlaji kwa mwezi Machi 2016 umepungua, hii ina maana kuwa sasa mtu
kuongeza ziada ili aweze kununua bidhaa na huduma sawa na zile alizokuwa na
uwezo wa kuzinunua mwezi Februari”

Kwa upande wa mfumuko wa Bei kwa nchi za Afrika Mashariki mwezi Machi,
2016, Kwesigabo amesema una mwelekeo unaofanana; Kenya umepungua kidogo
hadi kufikia asilimia 6.45 kutoka 6.84 huku Uganda ukifikia asilimia 6.2
kutoka asilimia 7.0 za mwezi Februari.
Picha na 2Waandishi wa Habari wakiwa kazini, wakati Ofisi ya Taifa ya Takwimu ikitangaza Mfumuko wa Bei Mwezi Machi 2016.
Picha na 1Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Ephraimu Kwesigabo akitoa taarifa ya kuongezeka  kidogo kwa mfumuko wa bei nchini kwa mwezi Mei 2016 leo jijini Dar es salaam.Mfumuko wa Bei mwezi Machi 2016 umepungua hadi asilimia  5.4  kutoka asilimia 5.6 iliyokuwepo Februari 2016.