Mke
wa Waziri Mkuu, Mary Majaliwa amefanya ziara katika Hospitali ya wilaya
ya Ruangwa mkoani Lindi na kutoa msaada wa mashuka kwa akinamama
waliojifungua.
Pia
ametumia fursa hiyo kuwapongeza madaktari na wauguzi wa Hospitali ya
wilaya ya Ruangwa kutokana na kuwahudumia vizuri wananchi na kuwaomba
waendelee kufanya kazi hiyo kwa mujibu wa maadili ya kazi yao.
Mke
wa Waziri Mkuu ameyasema hayo jana wakati alipotembelea wodi ya
akinamama waliotoka kujifungua na kufurahishwa na hali ya utoaji huduma
hospitalini hapo, ambapo aliwasisitiza kuendelea moyo huo kwa sababu
wao ndio wamebeba dhamana ya afya za wananchi.
“Nimefurahi
kukuta wazazi wanahudumiwa vizuri na wenyewe wamekiri kwamba huduma
zinazotolewa hospitalini hapa ni za kuridhisha, tofauti na tulivyozoea
kusikia wagonjwa wakiwalalamikia wauguzi, hivyo ni jambo la kujivunia,
hongereni sana” amesema.
Mmoja
wa wagonjwa waliolazwa katika wodi hiyo Hamisa Rashid ambaye amelazwa
katika wodi hiyo amesema alifikishwa hospitalini hapo wiki mbili
zilizopita akiwa katika hali mbaya na ameweza kuhudumiwa vizuri na sasa
anakaribia kutoka.
“Mimi
nilikuwa sijitambui, siwezi kufanya kitu chochote lakini baada ya
kuletwa hospitalini hapa madaktari kwa kushirikiana na wauguzi
wamenihudumia vizuri na sasa naweza hata kwenda chooni mwenyewe na bila
msaada wao mimi ningekuwa nimepoteza maisha kutokana na hali yangu
ilivyokuwa,” amesema Hamisa.
Mbali
na kutoa msaada huo wa mashuka pia ametoa baiskeli mbili kwa ajili ya
wanawake wawili walemavu lengo likiwa ni kuwawezesha kufanya shughuli
zao za kijamii kwa urahisi.
Akizungumza
baada ya kupokea msaada huo, Rehema Omary amemshukuru mke wa Waziri
Mkuu kwa msaada huo, ambapo alimuomba Waziri Mkuu, Majaliwa awawezeshe
kwenda kushiriki katika shughuli mbalimbali zinazofanywa na walemavu
ikiwemo michezo.
Kwa
upande wake Mkuu wa mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi amewataka watumishi wa
hospitali hiyo kufanya kazi kwa bidii na kuachana na utendaji kazi wa
mazoea kwa sababu umepitwa na wakati.
Pia
amesema amefurahishwa na kitendo cha wagonjwa kukiri kuwa wanahudumiwa
vizuri tofauti na hospitali zingine hivyo kuwataka kuendelea na ari
hiyo ya kufanya kazi kwa bidii, maarifa na weledi mkubwa.
Imetolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu
0 comments:
Post a Comment