NEWSPOINTTZ.BLOGSPOT.COM

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella Atoa Masaa 48 Kwa Watumishi Kuhamia Maeneo yao Ya Kazi



Mkuu  wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela ametoa saa 48 kuanzia leo kwa Wakuu wa Idara wa Halmashauri ya Misungwi ambao wana makazi yao Mwanza mjini kuhamia mara moja kwenye maeneo ya kazi.

Mongela alitoa agizo hilo jana wilayani Misungwi alipozungumza na watendaji wa kata na vijiji, madiwani na wakuu wa Idara wa halmashauri kwenye ziara yake ya kwanza ya kikazi tangu ateuliwe kuwa Mkuu mpya wa Mkoa wa Mwanza, na kubaini baadhi ya wakuu wa Idara wanaishi jijini Mwanza.

Alimuagiza Ofisa Usalama wa Taifa wa Wilaya(DSO) ya Misungwi, Stanslaus Mbile awafanyie uhakiki wa kina wakuu hao wa Idara kuhamishia makazi yao Misungwi ili wawahudumie wananchi kwa wakati.

“DSO nenda nyumba hadi nyumba za wakuu hawa wa Idara na uhakikishe kila mtu kwa kuwahesabu akiwa na familia yake wamehamia kwenye nyumba zao, nimekuagiza wewe kwa sababu unajua utaratibu wa vikao vyetu, ukishindwa kulisimamia hilo kikamilifu nitajua pa kukupeleka,” alisema Mongella.

Alisema haiingii akilini kwa mtumishi wa umma aliyeajiriwa na kuishi kwa mshahara unaotokana na kodi za wananchi akiishi nje ya eneo la kazi, jambo ambalo alisema litaleta shaka katika kuwahudumia wananchi.

“Siwezi mimi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, halafu naishi Shinyanga, huwezi kuwa DC wa Misungwi halafu unaishi Sengerema na kwa mtindo huu huwezi kuwahudumia wananchi,” alisema Mongella na kuongeza:

 “Kuanzia leo (jana) na Wakuu wa Idara wanaokaa nje ya Misungwi watumie siku ya Karume (jana) kuhamia Misungwi na niwaambie kuwa utaratibu wa Serikali ya Awamu ya Tano kila mtu awajibike kwenye kipande chake.”

Alisema hakuhamishiwa mkoani Mwanza kwa lengo la kuhubiri kifo au siku ya kustaafu kwa watumishi wa umma bali ameteuliwa na Rais John Magufuli kwenda mkoani Mwanza kufanya kazi za maendeleo ya wananchi na kushughulika na matatizo ya wananchi na kuyatafutia majawabu.

Aidha, alimuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Misungwi, Nathaniel Mshana kuhakikisha watendaji wa kata na vijiji wanaishi kwenye maeneo yao ya kazi ili iwe rahisi kwa wao kuwahudumia wananchi.
Share on Google Plus

News Point inakusogezea habari kubwa za kila siku kutoka kila kona ya dunia. Ungana nasi kupitia Facebook , Twitter na Instagaram ili uwe wa kwanza kupata habari.

0 comments:

Post a Comment