NEWSPOINTTZ.BLOGSPOT.COM

Obama: Tulikosea Sana Kuivamia Libya na Kumuondoa Muammar Gaddafi


Rais wa Marekani Barack Obama amekiri kwa mara ya kwanza kwamba serikali yake ilifeli katika kutatua mzozo wa Libya.

Amesema hilo huenda ndilo “kosa kubwa” zaidi alilolitenda wakati wa utawala wake.

Bw Obama amesema Marekani haikua na mpango mahususi wa jinsi taifa hilo litakavyotawaliwa baada ya kuondolewa madarakani kwa Kanali Muammar Gaddafi.

Alisema haya katika mahojiano na runinga ya Fox News kuangazia mafanikio na mapungufu ya utawala wake.

Hata hivyo ametetea hatua ya kuingilia kijeshi nchini Libya. Marekani na Muungano wa NATO zilitekeleza mashambulio ya anga kuwalinda raia baada ya kuzuka maasi dhidi ya Muammar Gaddafi mwaka 2011.

Lakini baada ya mauaji ya kiongozi huyo, Libya ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya makundi ya waasi huku makundi mawili yakiunda serikali na mabunge tofauti.
Katika hatua za kurejesha utulivu serikali ya muungano wa kitaifa inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa imewasili katika mji mkuu Tripoli ili kuanza mipango ya kuongoza nchi ya kurejesha hali ya kawaida.

Uchaguzi mkuu nchini Marekani utafanyika Novemba na Rais Obama atakabidhi madaraka kwa mrithi wake Januari mwakani baada ya kuongoza kwa mihula miwili.

Chanzo: BBC
Share on Google Plus

News Point inakusogezea habari kubwa za kila siku kutoka kila kona ya dunia. Ungana nasi kupitia Facebook , Twitter na Instagaram ili uwe wa kwanza kupata habari.

0 comments:

Post a Comment