Kampuni
kutoka Falme za Kiarabu, Rental Solutions and Services LLC imeiburuza
mahakamani kampuni ya kufua umeme ya Symbion Tanzania Limited, ikidai
kulipwa Dola za Marekani 228,070,655.67 ambazo ni zaidi ya Sh bilioni 560 kama fidia na malipo ya ukodishaji wa mitambo ya kuzalishia umeme nchini.
Kesi hiyo Namba 234 ya mwaka 2016 imefunguliwa katika Mahakama Kuu Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mdaiwa
wa pili katika shauri hilo ni Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco),
ambalo limeunganishwa katika kesi hiyo kama mdau mkuu kwenye sakata hilo
ambapo maamuzi yatakayotolewa na mahakama yanaweza kuiathiri.
Katika
hati ya madai, Kampuni ya Rental Solutions and Services inadai Symbion
Dola za Marekani 28,070,655.67 kama malimbikizo ya gharama za
ukodishwaji wa mitambo, ambayo hadi sasa Symbion imeshindwa kulipa na
pia katika shauri hilo Symbion itatakiwa kulipa Dola za Marekani milioni
200 ambazo ni fidia kwa kampuni hiyo kula hasara kutokana na Symbion
kuvunja masharti ya mkataba na kuchelewesha au kushindwa kufanya malipo
hayo.
Kwa
mujibu wa hati hiyo ya madai, fedha hizo zinatokana na kazi
zilizofanywa na kampuni hiyo ya Uarabuni ya kusambaza, kusimika na
kuendesha mitambo ya kuzalisha umeme ambayo ilikodishwa na Symbion kwa
matumizi ya miradi mbalimbali ya kuzalisha umeme kwa ajili ya Tanesco
ili usambazwe kwenye Gridi ya Taifa kama ilivyokubaliwa kwenye mikataba.
Rental
Solutions and Services pia katika kesi hiyo, inaiomba Mahakama kutamka
kuwa kushindwa kwa Symbion kulipa gharama hizo za ukodishaji kama
ilivyokubaliwa kwenye mkataba na pande zote mbili kumesababisha uvunjifu
wa mkataba na hivyo sio halali na haistahili kuendelea.
Inadaiwa
kuwa kati ya Septemba 2011 hadi Juni 2013, Rental Solutions and
Services iliingia mikataba mbalimbali na Symbion ambapo pale
ilipohitajika mikataba hiyo iliongezewa muda ili kukidhi mahitaji kwa
mujibu wa mikataba hiyo kwa lengo la kusambaza na kusimika mitambo ya
umeme ili kusambazwa kwenye Gridi ya Taifa.
Septemba
21, 2011 kampuni hiyo ya Uarabuni iliingia mkataba na Symbion kwa ajili
ya kusambaza na kusimika mitambo ya umeme katika Kituo cha Zuzu cha
Tanesco chenye nguvu ya kilovolti 33 kilichoko Dodoma yenye uwezo wa
kuzalisha megawati 50.
Katika
mitambo hiyo, pande husika zilikubaliana malipo ya Dola za Marekani
1,374,500 kwa mwezi kwa kipindi ambacho kingeishia miezi sita. Inadaiwa
kuwa kwa kipindi hicho, Symbion ingepaswa kulipa jumla ya Dola za
Marekani 8,247,000.
Hati
ya mdai inaonesha kuwa mkataba kama huo uliingiwa na pande zote mbili
Februari 12, 2012, kuhusu mitambo ya kuzalisha umeme wa megawati 55 kwa
kipindi cha miezi 12 kwa gharama ya Dola za Marekani 1,666,000 kwa
mwezi.
Mitambo
hiyo ipo katika vituo vya Arusha na Dodoma. Kwa mujibu wa hati ya
madai, kulikuwepo na ongezeko wa muda wa matumizi wa mitambo hiyo katika
vituo vya Dodoma na Arusha ambapo Rental Solutions and Services
ilitimiza matakwa yake kama ilivyo kwenye mikataba na iliwasilisha hati
za malipo kwa Symbion ili kukamilisha malipo ya kukodi kitambo hiyo kama
inavyotakiwa.
Pamoja
na Rental Solutions and Services kutimiza masharti ya mikataba hiyo,
kati ya Dola za Marekani 77,667,666.28, Symbion imelipa dola
49,597,010.61 tu. Hivyo, Rental Solutions and Services inadai kuwa hadi
sasa, bila uhalali wowote, Symbion imeshindwa kutimiza masharti ya
mkataba kwa kutolipa kiasi cha dola 28,070,655.67.
chanzo>mpekuzi
0 comments:
Post a Comment