Makamu
wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema serikali haina nia ya kumwonea
mtu, inapochukua hatua ya kutumbua majipu kwa watumishi wa umma.
Samia
aliyasema hayo juzi baada ya kupokea taarifa ya Mkoa wa Morogoro,
iliyosomwa na Mkuu wa Mkoa huo, Dk Steven Kebwe akiwa katika ziara yake
ya kikazi ya siku tatu mkoani humo.
Alisema
lengo la kutumbua majipu ni kurekebisha na kurejesha nidhamu, uadilifu
na uwajibikaji serikalini, kama ilivyoangizwa katika Ilani ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) ili Watanzania wote wafaidike na matunda ya nchi yao.
“Mtasikia
katika serikali tunarekebisha, majipu yanatumbuliwa... kwa kweli hatuna
nia ya kumwonea mtu, tunarekebisha kama ilivyoagizwa katika Ilani yetu
ya Chama Cha Mapinduzi ili Watanzania wote wafaidi matunda ya nchi yao,” alisema Samia.
Alisema
katika marekebisho hayo, serikali imechukua hatua ya kukata mishahara
ya walio juu na kunyanyua ya walio chini waje juu kidogo na kwamba
jitihada zote hizo ni katika kufanya mambo yaende vizuri nchini.
“Tunapozungumzia
amani na utulivu ni pamoja na kuhakikisha kwamba walio chini wapo
vizuri, wasipokuwa vizuri hakuna amani na utulivu, kazi itawapata watu
wa kamati ya ulinzi na usalama, kuwatuliza kila siku na hawatatulizika
kwa sababu wana shida,” alisema Makamu wa Rais na kuongeza: “Lakini
tukiwatuliza kwenye mambo yao wana maji, wana umeme, wana chakula,
mtoto anaenda shule vizuri, anapata afya, akienda zahanati dawa zipo,
watatulia tu.”
Alisema
kwa hivi sasa kuna tatizo la watumishi hewa na wengine wamediriki
kumdanganya mkuu wao wa kazi na hayo ndiyo mambo ambayo hayaleti picha
nzuri katika serikali.
Aliwataka
wakuu wa mikoa na wilaya nchini kuunga mkono jitihada hizo za serikali
ili kurejesha nidhamu na uwajibaikaji kwa watumishi wote. Wakati huo
huo, Makamu wa Rais ametembelea kiwanda cha kutengeneza nguo cha Mazava,
ambapo aliutaka uongozi wa kiwanda hicho kuzingatia masharti ya ajira
na wafanyakazi kuchapa kazi kwa bidii ili Taifa lipate kodi na wao
wapate mapato.
Akizungumza
na wafanyakazi, Samia aliuhakikishia uongozi wa kiwanda hicho kuwa
serikali itazifanyia kazi changamoto za eneo na ukosefu wa ujuzi kwa
kuwapeleka vijana wengi kwenye vyuo vya elimu ya ufundi stadi (VETA)
kujifunza ushonaji.
Alisema
Serikali ya Awamu ya Tano imeweka mkazo kwenye viwanda na kusisitiza
kwamba kupitia mpango wa EPZ, viwanda vingine vinatarajiwa kujengwa
mkoani humo, jambo ambalo litaongeza ajira kwa vijana.
Kiwanda
hicho ambacho kilianza uzalishaji mwaka 2010 kina wafanyakazi zaidi ya
2,000 na kwamba asilimia 100 ya nguo zinazozalishwa kiwandani hapo,
zinauzwa nje ya nchi, ambapo soko kuu liko Marekani.
0 comments:
Post a Comment