Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) January Makamba hii leo amekutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe wa Kamati ya Fedha ya Bunge la Finland.
Katika mazungumzo yao yaliyofanyika katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Luthuli Dar es Salaam, wabunge hao wameipongeza Serikali ya Tanzania kwa jitihada inazofanya za kulinda na kuhifadhi mazingira.

Awali, akiwakaribisha wabunge hao Waziri Makamba amesema Tanzania inajivunia uhusiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na Finland na kuwashukuru  wabunge hao kwa kufanya ziara hiyo ya kikazi nchini Tanzania.

Waziri Makamba amesema Serikali ya awamu ya Tano imejikita zaidi katika kuimarisha Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira ikiwa ni pamoja na kuandaa Mkakati Mkubwa wa Kitaifa wa kupanda miti nchi nzima hususan maeneo kame ili kunusuru nchi na athari za mabadiliko ya Tabianchi.

“Hivi sasa tuko katika hatua za kuainisha maeneo yatakayopandwa miti hiyo kwa kuangalia aina za udongo na miti itakayoweza kuhimili katika maeneo husika” Alisisitiza Makamba.

Waziri Makamba ameiomba Serikali ya Finland kuendelea kushirikiana zaidi na Serikali ya Tanzania ili kufikia malengo endelevu ya Uchumi na maendeleo ya Viwanda bila kuathiri Mazingira.

Naye Balozi wa Finland Nchini Tanzania Bw Mart Akhtsary aliyeambatana na ujumbe wa wabunge kutoka Finland amemhakikishia Waziri Makamba kuendeleza na kudumisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.
January Makamba
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais ( Muungano na Mazingira) January Makamba akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe wa Wabunge la Finland. Wabunge hao wa Kamati ya Fedha wamefanya mazungumzo na Waziri Makamba hii leo Ofisini kwake Mtaa wa Luthuli, Jijini Dar es Salaam.