NEWSPOINTTZ.BLOGSPOT.COM

Tanesco Mkoa Wa Pwani Yamakamata Mmiliki Wa Yadi Ya Magari Kwa Wizi Wa Umeme



Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Pwani limemkamata mmoja wa wamiliki wa eneo la maegesho ya magari la White Star, Munira Mbowe akidaiwa kujiunganishia umeme kinyume cha sheria.

Mbowe ambaye ni mmiliki wa eneo hilo lililopo Kiluvya kwa Komba nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, alikamatwa jana baada ya kufanyika msako wa kushtukiza kwa watu wanaodaiwa kujiunganishia umeme kinyume cha sheria.

Inadaiwa kuwa Mbowe amelisababishia shirika hilo hasara ya Sh50 milioni.

Akizungumza kwenye eneo hilo, Ofisa Usalama wa Tanesco Mkoa wa Pwani, Henry Byarugaba alidai kuwa baada ya kufanya ukaguzi waligundua umeme uliokuwa ukitumika katika eneo hilo haukuunganishwa na Tanesco.

“Tumekuwa tukibuni mbinu mpya kila kukicha ya kuwatia mbaroni wateja wetu wanaotuhujumu na leo (jana), tumembana huyu anayedaiwa ni mmiliki wa yard hii ya White Star baada ya kukuta anatumia umeme wa wizi uliounganishwa katika njia tatu,” alidai Byarugaba.

Alisema tayari wameshamfikisha Kituo cha Polisi Kibaha na hatua zingine za kisheria zinaendelea kuchukuliwa.

Hata hivyo, alidai kuwa hiyo siyo mara ya kwanza kwa Mbowe kukamatwa kwa kosa hilo. Alidai mwaka jana Tanesco ilipofanya msako, ilimkamata akiwa amejiunganishia umeme na alichukuliwa hatua za kisheria.

Alipoulizwa  kama tuhuma hizo zina ukweli, Mbowe alijitetea kuwa hajui ni nani aliyemuunganishia njia hizo tatu za umeme kwa sababu mara nyingi hufanya shughuli zake jijini Dar es Salaam, mara chache hufika kwenye yard hiyo kufanya kazi zingine ambazo ni chache.

“Ni kweli tumekutwa na kosa la kuiba umeme, lakini jamani nataka niwaeleze kuwa mimi sihusiki na kingine, nawaomba msinitoe kwenye vyombo vya habari, haya ni maisha tu, sio vizuri kunitoa jamani mimi sihusiki kabisa katika wizi huu,” alijitetea Mbowe.

Kaimu Meneja wa Taneso Mkoa wa Pwani, Selemani Mgwila alisema kitendo alichokifanya mteja wao huyo ni kosa kwani umeme waliokuwa wanautumia umesababisha upotevu wa mapato makubwa ya shirika.

“Tunalalamika kila siku mpaka shirika linaonekana halifanyi kazi kwa sababu ya hawa watu wachache, safari hii lazima sheria ichukue mkondo wake,” alisema.
Share on Google Plus

News Point inakusogezea habari kubwa za kila siku kutoka kila kona ya dunia. Ungana nasi kupitia Facebook , Twitter na Instagaram ili uwe wa kwanza kupata habari.

0 comments:

Post a Comment