Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amemtaka
mkandarasi Hainan International Limited anayejenga Daraja la mto Sibiti
ambalo linaunganisha mkoa wa Singida na Simiyu kuendelea na ujenzi
wake.
Amesema
hayo mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo na
kuwahakikishia wananchi kuwa daraja hilo litakamilika katika kipindi cha
hivi karibuni baada ya Serikali kuanza kumlipa mkandarasi huyo.
“Tumeanza
kumlipa mkandarasi fedha hivyo tunawahakikishia kwamba katika kipindi
kifupi kijacho litakamilika ili kufungua shughuli za kiuchumi kwa wakazi
wa Wilaya ya Mkalama na Meatu” , amesema Prof. Mbarawa.
Aidha
Waziri huyo wa Ujenzi , Uchukuzi na Mawasiliano amekemea tabia ya
baadhi ya wananchi kutoza ushuru katika mto huo na kusisitiza kwamba
tabia hiyo iachwe mara moja na atakayefanya hivyo anakiuka sheria na
hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
“Wananchi
wanatakiwa kupita hapa bila ya kulipa gharama yoyote katika mto huu,
nimemuagiza Mkuu wa Wilaya na Meneja wa TANROADS mkoa wa Singida
waboreshe eneo la kuvukia ili wakati ujenzi unaendelea huduma za kuvuka
ziendelee kama kawaida”, amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Naye
Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Singida Eng.
Leonard Kapongo amemhakikishia waziri kuwa ujenzi wa Daraja la mto
sibiti pia utahusisha barabara ya maingilio yenye urefu wa kilomita 25
inayounganisha wilaya ya Mkalama na Meatu.
“Ujenzi
wa barabara za maingilio unahusisha makalvati makubwa 10 na madogo 55
ili kuruhusu maji kupita kwa kasi na hivyo kudhibiti mafuriko”,
amefafanua Eng. Kapongo.
Kwa
upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Bw. Christopher Ngubiagai
amemshukuru Waziri Prof. Mbarawa kwa jitihada zake za kutaka kuunganisha
wilaya yake na Meatu kwani kukamilika kwa daraja hilo kutaimarisha
fursa za usafirishaji wa mazao na huduma za usafiri katika Wilaya hizo.
Zaidi
ya shilingi bilioni 18.2 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa Daraja
la mto Sibiti lenye urefu wa mita 82 na upana wa mita 10.5 ambapo tayari
Serikali imeshalipa zaidi ya shilingi bilioni 4 mpaka sasa.
Katika
hatua nyingine Prof. Mbarawa amekagua ujenzi wa nyumba za viongozi wa
Wilaya ya Mkalama na jengo la Halmashauri ya Wilaya hiyo na kuwataka
makandarasi wanaoendelea na ujenzi wa miradi hiyo kuongeza kasi na
kutumia fedha wanazopata kujenga jengo moja moja kwa awamu ili kupunguza
changamoto ya makazi na ofisi Wilayani humo badala ya utaratibu wa
sasa wa kujenga majengo yote kwa pamoja.
.”Msisubiri
mpate fedha zote kwa nyumba zote, kamilisheni ujenzi wa nyumba moja
moja kadri mnavyopata fedha ili kupunguza changamoto za makazi na
ofisi”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Prof.
Mbarawa yuko katika siku ya pili ya ziara yake ya siku nne mkoani
Singida ya kukagua miradi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, nyumba
na Mawasiliano.
Meneja
wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Singida Eng. Leonard
Kapongo (wa kwanza kushoto), akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (wa pili kushoto) kuhusu
mradi wa ujenzi wa Daraja la Mto Sibiti linalounganisha Wilaya ya
Mkalama mkoani Singida na Meatu mkoani Simiyu.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (wa pili
kushoto) akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara nchini
(TANROADS), mkoa wa Singida Eng. Leonard Kapongo (wa kwanza kushoto)
kuhusu usimamizi wa ujenzi wa Daraja la mto Sibiti.
Muonekano
wa moja ya nguzo inayoshikilia Daraja la Mto Sibiti linalounganisha
Wilaya ya Mkalama mkoani Singida na Meatu mkoani Simiyu.
Mkuu
wa Wilaya ya Mkalama Bw. Christopher Ngubiagai (katikati), akifafanua
jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa
(wa kwanza kushoto) alipokagua ujenzi wa Daraja la Mto Sibiti.
Muonekano
wa jengo la ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama inavyoonekana
katika hatua za awali za ujenzi wake. Zaidi ya milioni 758 zinatarajiwa
kutumika katika ujenzi huo.
Muonekano
wa juu wa Daraja la Msingi lenye urefu wa mita 75 linalounganisha
Wilaya ya Mkalama na Iramba, lililopo mkoani Singida.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (wa kwanza
kushoto) akikagua jengo la nyumba ya Mkuu wa Wilaya ya Mkalama
linalojengwa na Wakala wa Majengo nchini (TBA) mkoani Singida.
Muonekano
wa moja ya nguzo inayoshikilia Daraja la Mto Sibiti linalounganisha
Wilaya ya Mkalama mkoani Singida na Meatu mkoani Simiyu.
Imetolewa na kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
0 comments:
Post a Comment