NEWSPOINTTZ.BLOGSPOT.COM

CCM,MSAJILI WA VYAMA NA PROFESA WAPINGA ‘UKUTA’ YA MBOWE

SIKU moja baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutangaza nia ya kufanya mikutano ya hadharani nchini kote kuanzia Septemba Mosi kutokana na sababu mbalimbali, taasisi na wadau mbalimbali wamelaani mpango huo.

Akizungumzia hilo, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi amesema amepokea kwa masikitiko makubwa tamko hilo, huku Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikijitokeza na kulaani mpango huo.

Wengine waliopinga mpango huo ni wasomi wakiwemo Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anayejipambanua katika siasa za upinzani, aliyewahi kuwa mwanachama wa Chadema, Dk Kitila Mkumbo na wachambuzi wa Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk Benson Bana na Dk Bashiru Ally.

Msajili vyama vya siasa alaani

Akizungumzia tamko hilo la Chadema, Jaji Mutungi alisema limejaa lugha ya uchochezi, kashfa, kuudhi na lenye kuhamasisha uvunjifu wa amani.“Natumia fursa hii kukemea tamko hilo hadharani, kwa mujibu wa kanuni ya 6 (2) ya Kanuni za Maadili ya Vyama vya Siasa, pia nawaasa Chadema wasiendeleze tabia hii,” alisema Jaji Mutungi.

CCM wajibu mapigo

Katika hatua nyingine CCM imeionya Chadema kuacha kupotosha umma na kutaka kuwaaminisha wananchi uongo wanaoutunga ili kujaribu kupata wafuasi.Msemaji wa CCM, Christopher ole Sendeka alisema Dar es Salaam jana kuwa tamko lililotolewa na Chadema la kupanga kufanya mikutano ya hadhara nchi nzima kuanzia Septemba Mosi mwaka huu, limejaa uongo na ubabaishaji na linaonesha kuwa wapinzani wamekosa ajenda na njia pekee wanayoona inafaa ni kutunga utapeli, uongo na uzushi.

Wasomi UDSM wafunguka

Wakitoa maoni wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Mkumbo, Dk Bashiru na Bana walikosoa mpango huo wa Chadema. Profesa Mkumbo alisema vyama vya siasa vina wajibu wa kulinda misingi ya demokrasia lakini pia vina haki ya kupigania kufanya shughuli za siasa ingawa si kwa mapambano.

“Pande zote mbili yaani Jeshi la Polisi na vyama vya siasa vipeane nafasi kila mmoja, bila kuvuruga shughuli za maendeleo, kulindwa kwa demokrasia na kuiendeleza,” alisema Profesa Mkumbo.

 

Share on Google Plus

News Point inakusogezea habari kubwa za kila siku kutoka kila kona ya dunia. Ungana nasi kupitia Facebook , Twitter na Instagaram ili uwe wa kwanza kupata habari.

0 comments:

Post a Comment