NEWSPOINTTZ.BLOGSPOT.COM

MKAPA ATAKA AFRIKA IWE NA SERA TEKELEZI


 

RAIS mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, amezitaka nchi za Afrika kuhakikisha zinatoa kipaumbele katika uongozi unaojali masuala ya utawala bora, uzalendo na sera zinazotekelezeka ili kuweza kupata maendeleo endelevu.

Kwa mujibu wa Mkapa pamoja na marais wengine wastaafu wa nchi za Afrika, endapo nchi hizo zitashindwa kutumia njia sahihi kufikia malengo yake ya maendeleo zitajisababishia kuwa nchi zisizo na usawa katika mgawanyo wa mali na migogoro.

Akizungumza katika Kongamano la Viongozi wa Afrika lililofanyika jijini Dar es Salaam jana, Rais Mkapa alisema ni lazima Waafrika wajitume na kujiletea maendeleo yao wao wenyewe na kusisitiza kuwa hakuna mtu yeyote wa mataifa ya nje atakayewasaidia.

Alisema ni wakati muafaka sasa kwa Waafrika kuungana na kutumia uwezo walionao kuhakikisha ajenda ya Umoja wa Afrika (AU) ya kutafuta na kutumia rasilimali zinazopatikana Afrika ifikapo mwaka 2063 inafanikiwa.

“Kaulimbiu ya mwaka huu, inasema namna Sekta ya Biashara inavyoweza kuleta mageuzi Afrika kwa haraka. Kama mnavyojua katika ajenda yetu ya 2063 tumejiwekea malengo ya kuhakikisha nchi za Afrika zinakua kiuchumi na kuwa na maendeleo endelevu…lakini ili haya tuyafanikishe ni lazima tutegemee zaidi ushiriki wa Waafrika,” alifafanua.

Alitolea mfano kipindi cha uongozi wa Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere kwamba aliweka msisitizo katika masuala ya watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora ili kuwapatia maendeleo Watanzania.

Share on Google Plus

News Point inakusogezea habari kubwa za kila siku kutoka kila kona ya dunia. Ungana nasi kupitia Facebook , Twitter na Instagaram ili uwe wa kwanza kupata habari.

0 comments:

Post a Comment