Baada ya kulifanyia uchambuzi na kulitafakari tamko la Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, lililotolewa jana na msajIli mwenyewe, Jaji Francis Mutungi tumeona ni jambo lenye afya kwa ustawi wa demokrasia nchini, kusahihisha upotoshaji uliomo katika taarifa hiyo ili kuendelea kumsaidia msajili na watu wengine, watawala na walio sehemu ya utawala, kuelewa matakwa na maslahi ya wananchi hasa katika wakati huu ambao taifa linapitia.
Kwa hakika tumeshangazwa na kauli
zilizotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa, ambaye pia ni Jaji wa
Mahakama Kuu, kutokana na jinsi ambavyo anaanza kuonesha kuyumba katika
kutimiza wajibu wake hasa kwa kutumia weledi na ujuzi wake wa sheria kwa
kiwango cha nafasi yake kama jaji.
Katika tamko lake alilolitoa jana na
kunukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari jana hiyo na leo, ameshindwa
kuonesha neno hata moja linaloashiria matusi, kashfa, uongo au hata
kuvuruga amani lililotolewa mbele ya waandishi wa habari juzi wakati
Chama kikisoma hadharani maamuzi ya kikao cha Kamati Kuu.
Ni jambo la kushangaza kuwa Msajili
Mutungi, Jaji wa Mahakama Kuu ameweza kuweka vifungu vingi vya kisheria
akidai kuwa vimevunjwa lakini hawezi kuonesha ushahidi wa namna
vilivyovunjwa au maneno yanayothibitisha kuvunja hizo sheria.
Hii si sahihi hata kidogo na inakuwa ‘serious’ zaidi inapofanywa na mtu mwenye weledi wa sheria wa kiwango cha Jaji Mutungi.
Hii si sahihi hata kidogo na inakuwa ‘serious’ zaidi inapofanywa na mtu mwenye weledi wa sheria wa kiwango cha Jaji Mutungi.
Wakati Jaji Mutungi akinukuu vifungu vya
sheria na kanuni akionekana dhahiri kuwa kuegemea na kuwatetea watawala
ambao wamedhihirisha kuwa wanatamani nchi irudi enzi za ‘ujima’ wa
fikra za chama kimoja, kwa sababu anazozijua mwenyewe amesahau au
ameshindwa au amefanya makusudi kwa sababu anazozjijua mwenyewe, kunukuu
kifungu cha 4(1) (e) cha maadili ya vyama vya siasa za mwaka 2007,
ambacho kinatoa haki kwa vyama vya siasa kuendesha shughuli zao za
kisiasa ikiwemo mikutano ya hadhara na maandamano kwa mujibu wa sheria.
Tulidhani kuwa Ofisi ya Msajili wa Vyama
vya Siasa ambaye si tu kwamba ni mlezi wa vyama vyote bali pia
anasimama kama mwamuzi wa mchezo wa mpira uwanjani, katikati ya timu
mbili uwanjani, angelisimamia kifungu hicho muhimu na kukitumia
kuwakemea na kuwaonya watawala, akiwemo Rais, Waziri Mkuu na Jeshi la
Polisi wasivunje sheria za nchi kuzuia shughuli za siasa nchini kwa
sababu yoyote ile kwa sababu hawako juu ya sheria za nchi hii.
Aidha, sasa tunaanza kushtuka na kuanza
kujiuliza maswali mengi kuhusu kasi ya Msajili wa Vyama vya Siasa
kujijengea utaratibu usiokuwa na kawaida kwa nafasi yake ya kisiasa na
kisheria, kuwa na kasi ya ajabu kutoa kauli au matamko yanayoonesha
kuwatetea/kuwalinda watawala wanapovunja sheria zinazosimamia vyama vya
siasa.
Jaji Mutungi amekuwa mahiri wa kuvikemea au hata kuvionya vyama vingine tofauti na CCM, kila vinapodai haki za kisiasa ambazo ziko na zinapaswa kutekelezwa kwa mujibu wa sheria, wala si kwa hisani ya mtu yeyote.
Jaji Mutungi amekuwa mahiri wa kuvikemea au hata kuvionya vyama vingine tofauti na CCM, kila vinapodai haki za kisiasa ambazo ziko na zinapaswa kutekelezwa kwa mujibu wa sheria, wala si kwa hisani ya mtu yeyote.
Waandishi wa habari na umma kwa ujumla
watakuwa mashahidi kwa namna ambavyo CCM wamekuwa wakitumia vyombo vya
dola, kuvikandamiza, kuvinyanyasa, kuviwekea mazingira magumu na
kuvinyima haki za kufanya siasa vyama vingine washindani wake kwa ajili
tu ya kulinda maslahi ya chama kilichoko madarakani.
Katika hali hiyo ambayo hata imekuwa
ikisababisha mauaji na umwagaji damu za watu wasiokuwa na hatia kwa
sababu tu ni wafuasi wa vyama vingine, Msajili wa Vyama vya Siasa
hajawahi kuthubutu kujitokeza hadharani kuwaonya na kuwakemea CCM na
walioko serikalini kuwa kutumia vyombo vya dola kwa manufaa yao ya
kisiasa ni kosa kwa mujibu wa sheria za nchi kupitia kifungu cha maadili
ya vyama vya siasa cha 5(1)(c), za mwaka 2007.
Tulitegemea kwa kutumia umahiri huo huo
wa kunukuu vifungu vya sheria na kanuni za maadili ya vyama vya siasa
ambao Msajili amekuwa akiuonesha dhidi ya vyama washindani wa CCM kila
vinapodai haki za msingi za kisiasa, angekuwa ameutumia pia kuwakemea,
kuwaonya au hata basi kuwakumbusha CCM na Rais Magufuli kwa kutumia
kifungu cha 5(1) (i) cha kanuni za maadili ya vyama vya siasa za Mwaka
2007, kuwa ni makosa kutumia mamlaka, rasilimali za serikali, vyombo vya
dola au wadhifa wa kiserikali, kuvikandamiza vyama vingine kwa manufaa
ya kisiasa ya upande mmoja.
Si hayo tu, Jaji Mutungi ama aliamua kuwa kimya au alikuwa na kigugumizi aliposikia;
- Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Rais John Magufuli na Jeshi la Polisi wakitoa kauli kinyume cha sheria wakitangaza na kuagiza kuzuia shughuli za kisiasa nchini kwa matakwa yao tu.
- Mabalozi na wanadiplomasia wakizuiwa kukutana na asasi zisizo za kiserikali au vyama vya siasa.
- Kukiukwa kwa misingi ya sheria, kanuni na taratibu za nchi katika uteuzi wa wakurugenzi na makatibu tawala.
- Hali tete inayoendelea Zanzibar baada ya watawala kuharibu uchaguzi mkuu mwaka jana kisha wakafanya uchaguzi wa marudio kwa maslahi ya CCM, kinyume kabisa na sheria za nchi.
Hayo ni baadhi tu ya masuala ya muhimu
ambayo ofisi ya msajili ilitarajiwa kuwa ingekuwa mstari wa mbele
kukemea na kuonya ili kuweka mizania ya ushindani wa kisiasa katika
usahihi wake.
Kwa mwenendo huu ambao usipoangaliwa na
kufanyiwa kazi ya kuurekebisha haraka, tunachelea kusema kuwa Ofisi ya
Msajili na Jaji Mutungi mwenyewe wataanza kujikosesha uhalali machoni pa
Watanzania ambao wasingependa kuona siasa ambayo ni maisha yao,
ikifananishwa kama vile ni jambo la kawaida tu lisilokuwa na maana.
Kupitia taarifa hii, tunamtaka Msajili
wa Vyama vya Siasa, Jaji Mutungi kuwa makini na utaratibu huo vinginevyo
Watanzania wataanza kuiweka ofisi yake na yeye mwenyewe kwenye kapu
moja na aliyekuwa mtangulizi wake, ambaye ilifika mahali wananchi
walimuona yeye binafsi, kupitia kauli zake, matendo yake na ofisi yake
kwa ujumla, sawa na sehemu ya chama kilichoko madarakani.
CHADEMA kama chama kikuu cha upinzani nchini hakiwezi kuvumilia wala kukubali hiki kinachoanza kujionesha kuwa ni ‘double standards’ za
mtu anayetarajiwa kuwa mlezi na refarii, kujitokeza hadharani pale tu
ambapo maslahi ya chama tawala na watawala yanapoguswa lakini anakuwa
kimya na hata kuweka masikio nta mara vyama washindani wa CCM
vinapokandamizwa, kinyume kabisa cha sheria.
Kama chama chenye wanachama na viongozi
wanaojua haki na wajibu wao wa kikatiba na kisheria, tutaendelea kufanya
shughuli za kisiasa kwa namna itakayosimamia haki na matumaini ya
wananchi kwa ajili ya amani na utulivu wa kweli, kwa kuzingatia sheria,
kanuni na taratibu za nchi si kwa kufuata matamko, kauli au maelekezo ya
mtu yeyote.
Ni kwa kuzingatia dhana hiyo, maana
Kamati Kuu katika kikao cha dharura kilichofanyika mwishoni mwa juma
lililopita na maazimio yake kutangazwa juzi Jumatano, moja ya maazimio
yake ni kuanzisha operesheni ya UKUTA (Umoja wa Kupinga Udikteta
Tanzania) ambayo inalenga kuwaunganisha Watanzania wote bila kujali
tofauti zao zozote zile, kudai haki na matumaini dhidi ya udkiteta
katika nchi yao na kuzuia harakati za watawala kuataka kupora mamlaka ya
wananchi na kujiweka juu ya sheria kwa namna ile ile ambayo madikteta
hufanya.
Imetolewa leo Ijumaa Julai 29, 2016 na;
Prof. Mwesiga Baregu
Mjumbe wa Kamati Kamati Kuu
0 comments:
Post a Comment