Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe
29 Julai, 2016 ameanza ziara ya siku nne katika mikoa ya Singida,
Tabora, Shinyanga na Geita akitokea mkoani Dodoma, ambapo amezungumza na
wananchi kwa lengo la kuwashukuru kwa kumpigia kura katika Uchaguzi
Mkuu wa mwaka jana na kueleza juhudi zinazofanywa na serikali katika
kutatua kero za wananchi na kuwaletea maendeleo.
Akiwa
Mkoani Singida, Rais Magufuli aliyeongozana na mkewe Mama Janeth
Magufuli amewasihi watanzania kufanya kazi kwa juhudi na kujiepusha na
vitendo vya vurugu vinavyohamasishwa na baadhi ya wanasiasa huku akionya
kuwa serikali yake haitamvumilia mtu yeyote ambaye atathubutu kuchochea
vurugu ikiwemo maandamano kinyume cha sheria.
“Sitaki
nchi hii iwe ya vurugu, watakaoleta vurugu mimi nitawashughulikia
kikamilifu bila huruma, na wasije wakanijaribu, mimi ni tofauti sana na
kama wapo watu wanaowatumia wakawaeleze vizuri, mimi sijaribiwi na wala
sitajaribiwa.
“Wananchi hawa wana shida, na siasa nzuri ni wananchi washibe, siasa nzuri ni wananchi wetu wapate dawa” Amesema Rais Magufuli.
Kuhusu
hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali yake ya awamu ya tano
tangu aingie madarakani Rais Magufuli ametaja baadhi ya hatua hizo kuwa
ni kufuta ada kwa shule za msingi na sekondari, kutoa mikopo kwa
wanafunzi wa vyuo vikuu zaidi ya laki moja na kuongeza fedha za miradi
ya maendeleo katika bajeti ya serikali kutoka asilimia 26 ya mwaka
2015/2016 hadi kufikia asilimia 40 katika bajeti ya mwaka huu 2016/2017.
Hatua
nyingine ni kuondoa wafanyakazi hewa 12,500 katika orodha ya waliokuwa
wanalipwa mshahara na serikali, kudhibiti upotevu wa mapato serikalini,
kutenga shilingi Trilioni moja kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Reli ya
kati kwa kiwango cha kisasa yaani Standard gauge na pia akazungumzia
hatua zilizochukuliwa dhidi ya wala rushwa na wanaojihusisha na ufisadi
kwa kuunda mahakama ya mafisadi huku akiapa kuwa katika kipindi chake
hakuna fisadi atakayeendelea kutamba.
Akiwa
njiani Rais Magufuli amewasalimu wananchi wa Ikungi na baadaye amefanya
mkutano wa hadhara Singida Mjini ambako amesisitiza kuwa serikali yake
haiko tayari kumvumilia mtu yeyote atakayekwamisha utekelezaji wa Ahadi
na Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Singida
29 Julai, 2016
Rais huyo jaman wananchi wenzangu pumpe kero zetu
ReplyDelete