NEWSPOINTTZ.BLOGSPOT.COM

Serikali yajipanga kusitisha kubadili Vyuo vya Ufundi kuwa Vyuo Vikuu

Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imejipanga kusitisha zoezi la kubadili Vyuo vya Ufundi kuwa Vyuo Vikuu kwa nia ya kuinua vijana, kukuza na kuimarisha mafunzo ya ufundi stadi nchini.

Hayo yamesemwa jana na Naibu Waziri wa Wizara ya Kazi, Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu. Antony Mavunde alipoalikwa kama mgeni rasmi katika mahafali ya kwanza ya vijana waishio katika mazingira magumu yaliyofanyika katika Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), jijini Dar es Salaam.

Mhe. Mavunde alisema kuwa Serikali imeshaanza kuchukua hatua za awali za kuimarisha elimu na stadi mbalimbali za ufundi nchini ambapo moja ya hatua hizo ni kusitisha utaratibu wa kuvibadili vyuo vya ufundi kuwa vyuo vikuu na imefanya hivyo kwa sababu ya kutambua umuhimu na mahitaji makubwa ya wataalamu wanaohitimu katika vyuo hivyo kwenye soko la ajira.

“Serikali itaendelea kusimamia sera ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi ya mwaka 1994 ambapo pamoja na mambo mengine, sera hiyo inaweka msisitizo katika kuweka mazingira na kutoa elimu ya ufundi stadi katika ngazi mbalimbali ili kuendana na mahitaji ya mafundi sanifu nchini”, alisema Mhe. Mavunde.

Naibu Waziri huyo aliongeza kuwa amefarijika sana kuona vijana wamepatiwa mafunzo ya elimu ya ujasiriamali, stadi za maisha pamoja na kuunda vikundi vyao vya kuweka na kukopa ambavyo ni muhimu sana kwa wakati huu ambao Tanzania ya Viwanda inaandaliwa.

Pia alitoa rai kwa wazazi wenye vijana walemavu kuhakikisha wanatoa ruhusa kwa vijana hao kuungana na vijana wengine kushiriki katika fursa mbalimbali zinazotokea ili nao waweze kujenga uchumi wa Taifa.

Aidha, Mhe. Mavunde aliiomba Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kujitolea  kuwasaidia vijana hao kwa kuwapa elimu juu ya Mifuko hiyo ili watambue umuhimu wa kuhifadhi fedha zao ambazo zitakuja kuwasaidia uzeeni.

Elimu ya vijana waishio katika mazingira magumu ni Mradi wa miaka mitatu unaofadhiliwa na Umoja wa Jumuiya ya Nchi za Ulaya na kutekelezwa na Shirika lisilokuwa la kiserikali la Plan International, mradi huo unagharimu kiasi cha Euro 3,874,984.53 na unatekelezwa katika Mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Pwani, Lindi na Mtwara
Share on Google Plus

News Point inakusogezea habari kubwa za kila siku kutoka kila kona ya dunia. Ungana nasi kupitia Facebook , Twitter na Instagaram ili uwe wa kwanza kupata habari.

0 comments:

Post a Comment