Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amepokea
taarifa inayoelezea utaratibu uliotumika kumhamisha faru John kutoka
Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Sasakwa Black Rhino Sanctuary iliyoko
kwenye Hifadhi ya Grumeti.
Akizungumza katika kikao kilichofanyika
nyumbani kwake Oysterbay leo mchana na kuhudhuriwa na Waziri wa
Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe na baadhi ya watendaji wa
wizara yake, Waziri Mkuu amesema taarifa hiyo itafanyiwa kazi na
wataalamu wa ofisi yake.
Akisoma taarifa hiyo mbele ya Waziri
Mkuu, Profesa Maghembe amesema hadi kufikia Desemba 2015 wakati Faru
John anahamishwa alikuwa na watoto 26 (sawa na asilimia 70.2) ya faru
wote waliokuwepo ndani ya kreta.
“Uamuzi wa kumuondoa John ulikuwa ni
muhimu ili kuwezesha kuongezeka kwa faru weusi na kupunguza tatizo la
‘inbreeding’ ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro,” alisema Waziri Maghembe.
Baada ya kuhamishiwa Sasakwa, Waziri
Maghembe alisema Julai 10, 2016 afya ya faru John ilianza kudorora na
alikufa tarehe 18 Agosti, mwaka huu. Taarifa hiyo iliandaliwa na Kamati
ya Taifa ya kuwalinda tembo na faru. Kamati hiyo inaundwa na Mkurugenzi
Mkuu wa Tawiri, Mkurugenzi Mkuu wa Tanapa, Mkurugenzi Mkuu wa NCAA na
Mhifadhi Mkuu wa Ngorongoro.
Akikabidhi pembe za faru huyo mbele ya
Waziri Mkuu, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Kupambana na
Ujangili wa Wanyamapori, Robert Mande alimweleza kwamba pembe kubwa ya
faru John ilikuwa na uzito wa kilo 3.6 na pembe ndogo ilikuwa na uzito
wa kilo 2.3.
Watendaji wa wizara waliohudhuria kikao
hicho ni Kaimu Katibu Mkuu, Iddi Mfunda; Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya
Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Freddy Manongi; Mkurugenzi Mkuu wa Tawiri,
Simon Mduma; Kaimu Mkurugenzi Idara ya Wanyamapori, Alexander Songorwa
na Mkuu wa Pori la Akiba la Ikorongo/Grumeti, Nollasco Ngowe.
Desemba 6, mwaka huu, akiwa ziarani
mkoani Arusha, Waziri Mkuu aliuagiza uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya
Ngorongoro (NCAA), umletee nyaraka zote zilizotumika kumhamisha faru
maarufu kwa jina la ‘John’ kutoka kwenye hifadhi hiyo ifikapo Alhamisi,
Desemba 8.
News Point inakusogezea habari kubwa za kila siku kutoka kila kona ya dunia. Ungana nasi kupitia Facebook, Twitter na Instagaram ili uwe wa kwanza kupata habari.
RELATED POSTS
TAARIFA ZA KIFO CHA FARU JOHN ZATUA MIKONONI MWA MAJALIWA
Reviewed by Newspointtz
on
08:49:00
Rating: 5
0 comments:
Post a Comment