Watu
wasiojulikana maarufu kama mazombi wameivamia ofisi ya Chama cha
Wananchi (CUF) katika Jimbo la Dimani Wilaya ya Magharibi B.
Katika
tukio hilo lililotokea saa 6.30 usiku wa kuamkia jana, inadaiwa mazombi
hayo yalipora mali, kujeruhi watu na kuwateka wengine wa nyumba jirani
na ofisi hiyo.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Hassan Nassir Ali alithibitisha
kuwepo kwa tukio hilo huku CUF wakitaka uchunguzi uanze mara moja
kuwabaini wahalifu.
“Ni
kweli taarifa tunazo za watu kuvamia ofisi hiyo ya CUF na kuwapiga
pamoja na kuwahujumu watu na huo ni uharamia unaoripotiwa mara kwa
mara,” alisema Kamanda Ali.
Katika
tukio hilo, watu hao walioripotiwa kuwa na bunduki na silaha za jadi
kama mashoka, mapanga, mashanuo, chupa, spoku za baiskeli na nyundo,
walidaiwa kuvunja milango ya jengo la ofisi hiyo katika kijiji cha
Bweleo kabla ya kutembeza kipigo kwa majirani na kuondoka na vitu
kadhaa.
Katika
tukio hilo inadaiwa mazombi walitoweka na watu kadhaa akiwamo
Mwenyekiti wa CUF Tawi la Bweleo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Wazee wa chama hicho Wilaya ya Magharibi, Juma Ali Juma.
Akilaani tukio hilo, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma wa CUF, Salim Abdallah Bimani alisema,
“Huu ni uvunjifu wa amani na tunataka Rais John Magufuli iwapo anayo
nia ya dhati afuatilie hujuma hiyo ambayo watekelezaji wake wanajulikana
lakini hawakamatwi.”
Bimani alisema, “Mazombi
wameshawapiga sana wananchi hasa wafuasi wa CUF ambao hawana hatia,
wengine mpaka walipo-teza maisha, wameshawapiga watu na kuwajeruhi
vibaya na pia kuwaibia watu mali zao na hatuoni hatua yoyote
ikichukuliwa.”
Bimani alisema, “Tunamwambia Rais Magufuli kwa mujibu wa Katiba yeye ndiye mwenye mamlaka ya kuwalinda raia wote wa nchi hii, achukue hatua.”
Naibu
Mkurugenzi wa Haki za Binadamu wa CUF, Pavu Juma Abdalla aliwataja
waliojeruhiwa kutokana na vipigo vikali kuwa ni pamoja na Juma Shani
Mwita, Ali Saleh Shani, Kessi Khatib na Ame Mahmoud, wote wakazi wa
Bweleo.
Pavu alisema kuwa tukio hilo liliripotiwa katika Kituo cha Polisi cha Fumba na wahusika walipewa RB Na.18/2017.
Kwa
mujibu wa Mkurugenzi huyo inadaiwa kuwa miongoni mwa mali walizotoweka
nazo ‘mazombi’ kutoka ndani ya ofisi hiyo, ni simu nne, fedha taslimu
Sh300,000, viti 20, kifaa cha kudhibiti umeme, friji na bendera na
mlingoti wake.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Hassan Nassir Ali alisema, “Ni kweli
taarifa tunazo za watu kuvamia ofisi hiyo ya CUF na kuwapiga pamoja na
kuwahujumu watu na huo ni uharamia unaoripotiwa mara kwa mara.”
Nassir alisema,
“Pamoja na juhudi tunazozichukua ili kuukomesha kwa kushirikiana na
vikosi vingine, inaonekana hauwezi kuondoka kwa mara moja.”
Alisema kuwa jana walifanikiwa kuwashikilia watu wawili ili kusaidia polisi wakati ambapo jeshi hilo likiendelea na upelelezi.
Shambulio
hilo lilitendeka saa chache baada ya makamu mwenyekiti mstaafu wa CUF,
Juma Duni Haji na Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea kuwasili
Dimani ili kuendelea na kampeni za kumnadi mgombea wao, Abdulrazaq
Khatib Ramadhan.
0 comments:
Post a Comment