CHAMA
cha Wananchi (CUF) kimedai kuibiwa fedha za ruzuku zaidi ya Sh milioni
369 huku chama hicho kikiwahusisha waliokuwa viongozi wa chama hicho,
akiwemo Mwenyekiti wao, Profesa Ibrahim Lipumba na Mbunge wa Kaliua,
Magdalena Sakaya.
Aidha
chama hicho kimemuomba Rais John Magufuli, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,
Gavana wa Benki Kuu (BoT), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru), Ofisi ya Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na vyombo
vingine vinavyohusika, kuchukua hatua za dharura za kuokoa fedha hizo.
Hata
hivyo, Sakaya ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF upande wa Bara,
alisema fedha hizo hazijaibiwa kama ambavyo inadaiwa, isipokuwa kwa
nafasi aliyonayo ndani ya chama alimuandikia Msajili kuomba fedha hizo
kwa ajili ya chama kuingia katika uchaguzi, ndipo zikaingizwa katika
akaunti hiyo.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Saalam jana, Mwenyekiti wa Kamati
ya Uongozi, Julius Mtatiro alisema CUF imeibiwa Sh 369,378,502.64 za
ruzuku.
“Fedha
hizo zilitoroshwa kutoka Hazina ya Serikali Januari 5 mwaka huu na
kuingizwa kwenye Akaunti ya NMB tawi la Temeke yenye jina la The Civic
United Front ikiwa na akaunti namba 2072300456,” alisema Mtatiro.
Alisema
katika tukio hilo la wizi, Hazina imetorosha ruzuku hiyo kwa kumuamini
Lipumba, Sakaya, aliyekuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la CUF,
Thomas Malima na genge lao ambao walishavuliwa uongozi na pia uanachama.
Hata
hivyo, Mtatiro alisema kuwa baada ya kugundua utoroshwaji huo, CUF
imejiridhisha kuwa akaunti ambayo Hazina wameshiriki kuitumia kutorosha
fedha za umma na mali ya CUF ni akaunti ya CUF, ambayo hutumiwa na
Wilaya ya Temeke kwa ajili ya kupokea mgawo wa ruzuku kutoka kwa Chama
Taifa.
Aidha,
Mtatiro alisema vikao vya kitaifa vya CUF, yaani Kamati ya Utendaji ya
Taifa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, havikuwahi kupitisha maamuzi
yoyote kwamba fedha za CUF ziwekwe katika akaunti hiyo ya wilaya iliyoko
NMB Temeke.
Mtatiro
alisema siku mbili kabla ya utoroshaji wa fedha hizo, ulisukwa mpango
wa kuwaondoa baadhi ya viongozi wa CUF wa Wilaya ya Temeke kwenye utiaji
saini unaoihusu akaunti tajwa; na kuwafanya watu wa Profesa Lipumba
kuwa watia saini, ambao ni Sakaya na Malima.
Alisema
watia saini hao wapya, waliulizia kiasi cha fedha kilichomo kwenye
akaunti hiyo na walifanya hivyo katika tawi la NMB Mandela Road.
Alisema
kesho yake, wakiongozwa na Malima walikwenda katika Benki ya NMB tawi
la Temeke na wakatoa Sh milioni 69 na kuhamisha Sh milioni 300 kwenda
kwenye akaunti ya mtu binafsi kwenye akaunti ya NMB 41401600207
ikimilikiwa na Diwani wa CUF wa Handeni mkoani Tanga.
“Mtu
huyu ni wa karibu na Lipumba na ni mmoja kati ya wanachama wanane
waliosimamishwa uanachama na Baraza Kuu, jana (juzi) akaunti hii ilikuwa
kwenye mchakato wa kuondoa fedha hizo kutoka kwenye akaunti hiyo, na
kubaki na Sh 207,907 tu,” alisema Mtatiro.
Alisema
mtu huyo alitoa Sh milioni 100 kutokea Benki ya NMB tawi la Magomeni,
kisha akiwa hapo Magomeni akatoa Sh milioni 50, tawi la Kariakoo alitoa
Sh milioni 100 na mwisho akatoa tena Sh milioni 49.5 huku wakiwa na
ulinzi wa polisi na gari ya chama hicho akiwa na Sakaya na wengine.
“Hadi
tuongeavyo sasa miezi mitano CUF inadai ruzuku ya Shilingi milioni 635
na kwa kuwa fedha zilizotoroshwa Hazina zimepelekwa kwenye akaunti
isiyotambuliwa Bodi ya Wadhamini ya chama inatamka kuwa hadi sasa ruzuku
yake ni Shilingi 635,000,000,” alisema Mtatiro.
Mtatiro
alisema Bodi ya Wadhamini ya CUF inakutana na pia Kamati ya Utendaji ya
Taifa ya CUF pia kwa ajili ya kutafakari tukio hilo kubwa la chama na
kuelekeza hatua za kiutawala na kisheria za kuchukua haraka.
Jana Sakaya
alisema chama kimepata nafasi ya kushiriki uchaguzi mdogo katika kata
14 kati ya 20 za Tanzania Bara, hivyo fedha zinahitajika kwaajili ya
maandalizi hayo hivyo aliamua kumuandikia Msajili kuomba fedha.
“Hizo
fedha hazijaibwa wala nini, hao wanaoongea hawajui wanaongea nini, mimi
niliandika barua kwa nafasi yangu kulingana na uchaguzi tulionao mbele
yetu nikaomba hizo fedha na zimetolewa kwaajili ya kusambazwa
zinakohitajika,” alisema Sakaya ambaye alisema yuko jimboni kwake.
Sakaya
alisema taarifa zilizotolewa na Mtatiro, hazina ukweli na kwamba
Mtatiro hana nafasi yoyote ndani ya chama. Alisema ukweli ni kwamba
Msajili kuweka fedha kwenye akaunti hiyo ya tawi la Temeke ni sahihi,
kwani ana maamuzi ya kuweka popote ili mradi zinaingia katika akaunti
zinazomilikiwa na chama.
Aidha
alisema pia kuwa ni kweli fedha hizo zimetolewa na ni kwa ajili ya
kusambazwa katika halmashauri ambazo zinahitajika kuendelea na kampeni
za uchaguzi. Uchaguzi huo mdogo wa viti vya udiwani utafanyika Januari
22 mwaka huu.
Lipumba
pamoja na viongozi na wanachama wengine 10 Agosti mwaka jana
walisimamishwa uanachama na Baraza kuu la Uongozi la Taifa lililokutana
katika kikao cha dharura huko visiwani Zanzibar hata hivyo maamuzi hayo
yalitenguliwa na Msajili wa vyama vya Siasa.
Kikao
hicho pia kilimteua Mtatiro kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi
itakayokuwa na wajumbe wawili ambao ni Katani Ahmed Katani na Severina
Mwijage, ambayo itafanya kazi za Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti hadi
hapo utakapoitishwa Uchaguzi mwingine wa kujaza nafasi hizo.
0 comments:
Post a Comment