NEWSPOINTTZ.BLOGSPOT.COM

Rais Magufuli anatarajia kuanza ziara ya kikazi ya siku mbili Mkoani Simiyu kuanzia leo

Rais  John Magufuli leo anatarajia kufanya ziara ya siku mbili katika mikoa ya Simiyu na Shinyanga na atazungumza na wananchi kupitia mikutano ya hadhara, ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu achaguliwe kuwa Rais.

Katika ziara hiyo Rais Magufuli anatarajiwa kuweka jiwe la msingi katika Hospitali ya rufaa ya mkoa iliyopo mtaa wa Nyaumata na kufungua barabara ya Bariadi kwenda Lamadi ya urefu wa kilometa 50.3.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari jana Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka alisema kwa siku hizo mbili atafanya shughuli hizo na baadaye atazungumza na wananchi lengo kufahamu matatizo yao.

Alisema mkutano huo utafanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Somanda.

Mtaka alisema kuwa Rais Magufuli kwa siku ya kwanza atazungumza na wananchi wa mkoa wa Simiyu lilipowekwa jiwe la ufunguzi wa barabara hiyo, siku ya pili atatembelea kiwanda cha kutengeneza chaki kilichopo Maswa na baadaye ataweka jiwe la msingi katika barabara ya Mwigumbi-Maswa.Pia atazungumza na wananchi wilayani Maswa.

Aidha aliwataka wananchi mkoani hapa kujitokeza kwa wingi kumlaki na kumsikiliza Rais Magufuli ambaye hajawahi kufika mkoani humo tangu achaguliwe kuwa Rais.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainabu Telack, amesema Rais Magufuli anatarajia kufanya ziara ya siku moja mkoani kwake kesho na atazungumza na wananchi katika mikutano ya hadhara na kusikiliza kero zao.

Telack alisema kuwa ujio wa rais mkoani hapa ni kusherehekea siku ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo kitaifa zinafanyika kisiwani humo.

“Rais anatarajia kuwasili mkoani kwetu kwa ziara ya siku moja kwa lengo la kuzungumza na wananchi na siku hiyo itakuwa ni siku ya sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar hivyo atazisherekea akiwa mkoani hapa,” alisema.
Share on Google Plus

News Point inakusogezea habari kubwa za kila siku kutoka kila kona ya dunia. Ungana nasi kupitia Facebook , Twitter na Instagaram ili uwe wa kwanza kupata habari.

0 comments:

Post a Comment