Aliyekuwa
Wakala wa Kampuni inayodaiwa kuwa ni kampuni hewa ya kufua umeme wa
dharura, Richmond Development LLC, Naeem Gire ameachiwa huru baada ya
upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yake.
Akitoa
uamuzi huo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Hakimu
Mfawidhi, Cyprian Mkeha alisema upande wa mashitaka umeshindwa
kuthibitisha mashitaka mawili ya kughushi na kuwasilisha nyaraka za
uongo.
Uamuzi
huo ni wa pili kutolewa na mahakama hiyo dhidi ya mashitaka yaliyokuwa
yakimkabili Gire. Awali, aliachiwa huru baada ya kuonekana hana kesi ya
kujibu, ambapo Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) hakuridhika na uamuzi
huo na kukata rufaa Mahakama Kuu.
Katika
uamuzi wake, Mahakama Kuu ilisema haikuwa sahihi kumwachia, kabla
hajajitetea katika mashitaka ya kwanza na ya pili, ambayo ni kughushi na
kuwasilisha nyaraka za uongo. Hivyo, kesi hiyo ilirejeshwa Mahakama ya
Kisutu, na Gire akapanda tena kizimbani akajitetea na Hakimu Mkeha
ametoa uamuzi huo.
Katika
kesi hiyo hiyo, Julai 28, 2011 Gire aliachiwa huru katika mahakama hiyo
na Hakimu Mkazi, Waliarwande Lema kuwa hana kesi ya kujibu, lakini
Mahakama Kuu ilimtaka apande kizimbani tena kwa ajili ya kujitetea.
Katika
uamuzi wake wa kumwachia huru Gire, Hakimu Lema alisema kuwa ameridhika
na hoja za utetezi kuwa mshtakiwa huyo hana kesi ya kujibu, kwa kuwa
upande wa mashtaka umeshindwa kutengeneza kesi dhidhi ya mshtakiwa kwa
mashtaka yaliyokuwa yakimkabili, kiasi cha kumlazimu ajitetee.
Hakimu
Lema alisema baada ya kuupitia ushahidi uliotolewa mahakamani na
mashahidi wa upande wa mashtaka , hoja za pande zote na vifungu vya
sharia, aliridhika kuwa ushahidi huo hauna vigezo vya kuonesha kuwa
mshitakiwa huyo ana kesi ya kujibu.
Uamuzi
wa Mahakama Kuu ulitolewa na Jaji Lawrence Kaduri katika rufaa ya DPP
aliyekuwa akipinga uamuzi wa Mahakama ya Kisutu, kumwachia huru kuwa
hana kesi ya kujibu.
Jaji
Kaduri alisema kuwa baada ya kupitia ushahidi wa upande wa mashtaka,
ameridhika kuwa mshtakiwa huyo alikuwa na kesi ya kujibu na kwamba
ushahidi huo unamlazimisha apande kizimbani kujitetea.
Hata
hivyo, aliamuru mshtakiwa huyo arudi kizimbani katika Mahakama ya
Kisutu ili aanze kujitetea na kwamba kesi hiyo isikilizwe na hakimu
mwingine.
0 comments:
Post a Comment