Serikali inakusudia kuajiri watumishi wapya wa umma 52,436 katika mwaka ujao wa fedha.
Aidha,
madaktari wapya 258 waliokuwa waende kufanya kazi nchini Kenya, lakini
wakakwama kutokana na kuwekewa pingamizi la kimahakama na wenzao wao
huko na hivyo Rais, Dk John Magufuli kuamuru waajiriwe mara moja nchini,
wanatarajiwa kuanza kazi keshokutwa Jumatatu.
Hayo
yalisemwa bungeni juzi usiku na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
anayeshughulikia Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Angellah Kairuki alipokuwa anatoa ufafanuzi wa lini Serikali itaendelea
kuajiri watumishi wa kada nyingine, kama ilivyoulizwa na Mbunge wa Viti
Maalumu, Anna Lupembe (CCM).
“Azma
ya serikali, kwanza kabisa hatuwezi kuajiri wananchi wote, tumekuwa
tukisikia hapa wahitimu hawana ajira, wengine wanaendesha bodaboda…
tunapopanga idadi ya watumishi wa kuajiriwa, tunaangalia mambo mengi,
kuanzia mahitaji, vipaumbele hadi uwezo wa kibajeti.
“Tayari
tumeshaanza kutoa vibali vya ajira zaidi ya watu 9,700 na tutaendelea
kufanya hivyo, na hivi karibuni Rais amebariki kuajiriwa kwa madaktari
wapya 258 na Jumatatu (keshokutwa) wanaripoti kazini.
"Tutaendelea
kuajiri na wataalamu wa kada nyingine, kabla ya kumalizika kwa mwaka
huu wa fedha mwezi Juni tutakuwa tumejiajiri kwa idadi tutakayoipanga
kwa awamu, na katika mwaka ujao wa fedha tutaendelea kuajiri watumishi
wengine wa umma zaidi ya 52,436,” alisema.
Hata hivyo, alisisitiza Serikali itahakikisha hairudii makosa ya kuajiri watumishi hewa, wasio na sifa na weledi unaohitajika.
Alisema
kwa kiasi kikubwa uhakiki wa watumishi wa umma kwa ujumla umekwisha,
lakini kazi hiyo ni endelevu, kwani serikali itaendelea kufanya hivyo
mara kwa mara.
Alisema
matunda ya uhakiki wa watumishi wa umma umebaini watumishi hewa 19,708
na ambao wameshaondolewa katika orodha ya mishahara ya watumishi wa
umma.
“Hawa
wangeachwa, Serikali ingekuwa inapoteza kiasi cha Sh bilioni 19.8 kila
mwezi, lakini fedha hizi zimeokolewa kupitia uhakiki wa watumishi wa
umma.
"Tunafanya haya kwa nia njema. Mathalani tusingewatoa hawa, si wangeziba nafasi za ajira za wengine na fedha ngapi zingepotea?” alihoji.
Alisisitiza
kuwa, wizara hiyo itaendelea kutimiza majukumu yake kwa vitendo ili
kurejesha nidhamu ya serikali na utumishi wa umma kwa kuongeza uwazi na
kusimamia sheria, kanuni na taratibu za uwajibikaji wa viongozi wa
watumishi wa umma ili wawajibike kwa wananchi ambao ndio wateja na
waajiri wakuu wa watumishi wa umma.
Naye
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI), George Simbachawene, akijibu hoja za wabunge, hasa la
uhamisho wa watumishi wakiwemo wanandoa wanaotenganishwa, alikemea tabia
ya maofisa watumishi kuzuia wenye ndoa kuhama kutoka kituo kimoja cha
kazi kwa lengo la kuwafuata wenzao.
Alisema kuwazuia ni kuwanyima haki ya msingi, na kuwaagiza wabunge katika maeneo yao wasaidia kusimamia haki za watumishi.
"Lazima
sheria za utumishi zizingatiwe, walimu hawa au watumishi wanayo haki ya
kutoka sehemu moja kwenda nyingine, lakini pia kuishi na wenza wao,
lakini utadhani mtumishi anapoomba ni kama anasaidiwa, hapana ni haki
yake ya msingi, waheshimiwa tusimamie haki za watumishi,” alisema Simbachawene
0 comments:
Post a Comment