Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya
Tabora imeahirisha kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi Jimbo la Kigoma
Kusini iliyofunguliwa na aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, David Kafulila,
kupitia chama cha NCCR-Mageuzi akipinga ushindi wa Mbunge Hasna
Mwilima, wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kesi hiyo iliahirishwa jana na Jaji wa
mahakama hiyo, Ferdinand Wambali, baada ya Wakili wa kujitegemea,
Profesa Abdallah Safari, anamtetea mlalamikaji kuomba mahakama hiyo
impatie saa 48 ili akamilishe hati za kiapo za mashahidi wake watano na
baada ya hapo mahakama ipange tarehe nyingine ya kutajwa kwa ajili ya
kuanza kusikiliza.
Jaji Wambali alikubaliana na ombi hilo
na kusema hati za mashahidi zipelekwe kwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu
Kanda ya Tabora, Shanmillah Sanwatt, zikiwa zimefungwa kwenye bahasha
Machi 18, mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kigoma.
Alisema siku hizi kuna utaratibu
ulioanzishwa kwamba kila shahidi lazima awe na hati ya kiapo ndipo atoe
ushahidi wake mahakamani.
Aidha, Jaji Wambali alisema hati za
ushahidi zitakuwa zimefungwa na zitafunguliwa wakati wa shahidi
anapoanza kutoa ushahidi wake.
“Nia ya mahakama ni kutatua migogoro na
siyo kuongeza migogoro, hivyo jitahidini kuwasilisha hati za kiapo za
mashahidi ili kesi hiyo isikilizwe na kutolewa uamuzi haraka,” alisema
Jaji Wambali.
Alisema kutokana na matakwa ya
kisheria, upande wa mlalamikaji unatakiwa kuwasilisha hati za kiapo za
mashahidi zikiwa zimefungwa kwenye bahasha na zifikishwe hapo mahakamani
mapema iwezekanavyo ili kesi hiyo imalizike haraka.
Jaji Wambali aliwataka mawakili wa pande zote kuhakikisha siku ya kesi kusiwapo na upande wowote kutofika hapo mahakamani.
Aidha, Jaji Wambali aliuhoji upande wa
mshtakiwa unaoongozwa na Wakili wa Kujitegemea, Kennedy Fungamtama, kama
una pingamizi dhidi ya maombi ya upande wa mlalamikaji.
Hata hivyo, upande huo ulidai kuwa
hauna pingamizi dhidi ya maombi ya upande wa mlalamikaji na kuomba
tarehe nyingine ya kutajwa kwa ajili ya kuanza kusikiliza kesi hiyo.
Jaji Wambali alikubaliana na ombi hilo
na kuahirisha kesi hiyo hadi Machi 29, mwaka huu kesi hiyo itakapoanza
kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kigoma.
Katika kesi hiyo, Kafulila
atawakilishwa na Wakili Profesa Abdallah Safari pamoja na Tundu Lissu,
wakisaidiana na Wakili wa Kujitegemea Daniel Rumenyela.
Kwa upande wa Mbunge Mwilima,
atawakilishwa na Wakili wa Kujitegemea, Fungamtama pamoja na Mawakili wa
Serikali wanaomwakilisha Msimamizi wa Uchaguzi na Mwanasheria Mkuu wa
Serikali kama washtakiwa katika kesi hiyo.
Katika kesi hiyo, Kafulila anaiomba
Mahakama imtangaze kuwa mshindi kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi kifungu
Na. 112(c) kwa madai kwamba yeye ndiye aliyepata kura nyingi kulingana
na matokeo ya kila kituo kwenye fomu namba 21B na kwamba Msimamizi wa
Uchaguzi alimtangaza Mwilima kinyume cha matokeo halisi.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kigoma
jana ilifurika wanachama na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa na
watu wengine huku kukiwa na ulinzi mkali wa polisi waliokuwa na silaha
za moto na mabomu ya kutoa machozi.
News Point inakusogezea habari kubwa za kila siku kutoka kila kona ya dunia. Ungana nasi kupitia Facebook, Twitter na Instagaram ili uwe wa kwanza kupata habari.
RELATED POSTS
KESI YA KAFULILA YAPIGWA DANADANA
Reviewed by Newspointtz
on
14:34:00
Rating: 5
0 comments:
Post a Comment