MKAZI
wa Kijiji cha Ikondamoyo, Wilaya ya Mlele mkoani Katavi, Veronica
Salehe (54), aliyeoa wanaume wawili kwa kipindi cha miaka tisa amefariki
dunia.
Akizungumza
na waandishi wa habari juzi, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ikondamoyo,
John Maganga, alisema Veronica alifariki dunia wiki iliyopita mkoani
Tabora alikokuwa amekwenda kupatiwa matibabu kwa kaka yake.
Maganga alisema kuwa ndoa hiyo iliwezeshwa na mume mkubwa ambaye alikubali kuishi na mume mdogo.
Alisema
kuwa Veronica ndiye aliyewaoa wanaume wote wawili na kuishi nao kwa
miaka tisa, na kwamba ndiye aliyekuwa na amri kuu katika nyumba yao.
Aliwataja wanaume hao kuwa ni Paulo Sabuni (62) ambaye ndiye mume mkubwa na Arcado Mlele (47).
Maganga
alisema Veronica na mume wake mkubwa, walifika kijijini hapo miaka 24
iliyopita wakitokea Kijiji cha Usumbwa, mpakani mwa Chunya na Tabora.
“Baada
ya kufika kijijini hapa, walianza kujishughulisha na shughuli za kilimo
na biashara ya kuuza pombe za kienyeji aina ya komoni,” alisema Maganga.
Katika uhai wake, Veronica alibahatika kupata watoto wanne, kati yao wawili wa kike.
Maganga
alisema mtoto mdogo wa kiume, ni wa mume mdogo ambaye ana miaka tisa,
anayesoma darasa la nne katika Shule ya Msingi Ikondamoyo, na watoto
wengine watatu ni wa mume mkubwa.
Kuhusu
maisha ya Veronica ya kuishi na wanaume wawili, Maganga alisema haikuwa
siri kijijini hapo kwa sababu walizoeleka kwa wanakijiji.
Alisema
mume mdogo alikuwa anaishi kwenye nyumba aliyoachiwa na marehemu baba
yake, lakini alikuwa akishinda kwa mume mkubwa ambako kulijulikana zaidi
kwa jina la ‘nyumba kubwa’.
“Mambo ya kula, kunywa na mengine, mama alikuwa akiwapangia zamu kama afanyavyo mume mwenye wake wengi,” alisema Maganga na kuongeza kuwa wanaume hao walikuwa wanaridhika na kufurahia maisha.
Alisema
siku mama akichoka kupika, mume mdogo alikuwa akiingia jikoni na
kuwaandalia chakula watoto na mume mkubwa maji ya kuoga.
Wakati wa mazishi, wanaume wote walishiriki shughuli zote, jambo ambalo limeacha maswali mengi kwa jamii.
Akizungumzia
msiba huo, mume mkubwa alisema kuwa amepata pigo kubwa kwa sababu
alikuwa anasaidiwa mno na marehemu Veronica kutokana na biashara zake za
pombe za kienyeji ambazo zilisaidia kuendesha maisha ya kila siku.
0 comments:
Post a Comment