NDOA
iliyodumu kwa miaka tisa kati ya kampuni ya East Africa Power Poll na
serikali ya vijiji vya Kisasida na Ipungi manispaa ya
Singida,umevunjika rasmi baada ya serikali za vijiji hivyo kudai kwamba
kampuni hiyo imejaa ulaghai na hakuna mkataba waliowekeana.
Kampuni
hiyo ilikuwa iwekeze katika kuzalisha umeme wa upepo na iliishalipa
fidia yenye thamani ya zaidi ya shilingi 400 milioni kwa wakazi 197,
ili waweze kupisha mradi huo.
Katika
mkutano mkuu maalum wa vijiji hivyo ulioitishwa kuzungumzia mstakabali
wa kampuni hiyo,iliazimiwa kwa kauli moja kwamba hawaitambui tena. kwa
madai licha ya kutokuwa na mkataba,pia hakuna mihtasari wala nyaraka zo
zote katika ofisi za vijiji hivyo, inayoonyesha kampuni hiyo imeomba
uwekezaji.
Diwani
wa kata ya Mungumaji, Shaban Sato, akizungumza kwenye mkutano maalum wa
kujadili uhalali wa kampuni ya East Africa Power Poll kuwekeza katika
kuzalisha umeme wa upepo katika kijiji cha Kisasida.Pamoja na mambo
mengine,diwani huyo aliagiza watu waliolipwa fidia kupisha mradi wa
umeme wa upepo,warejee kwenye maeneo yao kwa madai kampuni ya East
Africa Power Poll haina mkataba na kijiji hicho.
Aidha,
kampuni hiyo imeagizwa isimamie yenyewe zoezi la kurejeshewa fedha za
fidia kwa watu waliowalipa,na kwamba serikali za vijiji
hivyo,hazitahusika kwa lolote lile.
Mwenyekiti
wa kijiji cha Kisasida, Hamisi Rupia,alisema kuwa baada ya kuingia
madarakani na kubaini kampuni hiyo haina mkataba na vijiji hivyo wa
kumilikishwa hekta 1,450,desemba 23 mwaka jana,aliiandikia barua ifike
ofisini kwake,ili waweze kuzungumzia uhalali wa umiliki huo.
“Lakini
hadi hivi sasa,kampuni hiyo haijawahi kujibu baraua hiyo,wala haijawahi
kutuma mwakilishi kuja kuelewana na viongozi wa serikali hizi mbili juu
ya umiliki wa eneo wanalolitaka kwa uwekezaji wao”,alisema mwenyekiti
wa kijiji cha Kisasida.
Diwani
wa kata ya Mungumaji (CCM),Shabani Satu,alipigilia msumari kampuni hiyo
kwa kudai kampuni hiyo imejaa ulaghai mtupu,na kuagiza watu ambao
wamelipwa fidia na kuyahama maeneo yao,warejee mara moja na kuanza
shughuli za kibinadamu.
Mwenyekiti
wa kijiji cha Kisasida manispaa ya Singida, Hamisi Rupia,(wa nne kutoka
kulia) akizungumza kwenye mkutano maalum uliokuwa na ajenda moja ya
mstakabali wa uwepo wa kampuni ka East Africa Power Poll iliyokuwa
iwekeze katika kuzalisha umeme wa upepo.
Diwani
huyo ambaye huko nyuma aliwahi kuwa mtetesi mkubwa wa kampuni hiyo na
kusimamia zoezi la kuorodhesha wakazi wanaostahili kulipwa fidia,alisema
kwa kipindi cha miaka tisa,ameshindwa kabisa kuielewa vizuri kampuni
hiyo kutokana na mwenendo wake,hivyo kwa watu waliolipwa fidia,watajuana
wao na kampuni hiyo.
Kwa
upande wake Ramadhani Yusuph,alisema kwamba kwa vile ofisi za serikali
za vjijiji hazina kumbukumbu ya mihtasari yo yote wa mikutano mikuu ya
vijiji hivyo inayoonyesha kuridhia uwekezaji wa hekta 1,450,kitendo
hicho pekee,kinainyima sifa kampuni hiyo kuwekeza.
“Kama
kweli wana nia ya dhati kuja kuzalisha umeme wa upepo kwenye maeneo
yetu,sisi hatuwezi kupigana na uwekezaji wa kitaifa.Waje waanze upya
kuomba kwa kuzingatia taratibu na sheria zilizopo”alisema.
Naye
Maulidi Simba,alisema fedha ya fidia aliyolipwa,haikuwa halali …..ni
ndogo sana tena ni ya kununulia bajia tu.Hivyo ameitaka kampuni hiyo
kumlipa fidia stahiki kwa kumsimamisha kuendelea na shughuli za
uzalishaji kwa kipinid cha zaidi ya miaka tisa.
Juma
Maluja, akitoa nasaha zake mbele ya mkutano mkuu maalum ulioitishwa
kujadili uhalali wa kampuni ya East Africa Power Poll kuwekeza kijijini
hapo kwa ajili ya kuzalisha umeme wa upepo.
Akizungumzia
sakata hilo, Afisa ardhi mteule manispaa ya Singida,Christian
Kasambala,alisema kuwa mgogoro huo ulioibuka upya,kwa kiasi kikubwa
unachangiwa na wanasheria wa vichakani, ambao ni wapotoshaji wakubwa.
“Maombi
ya uwekezaji ngazi ya kitaifa,hayatumwi au hayaombwi katika ngazi ya
serikali za vijiji, serikali za vijiji hazina ardhi…ardhi inamilikiwa na
mtu mmoja mmoja. Kisheria maombi hayo yanatumwa katika ngazi ya
halmashauri na nakala inapelekwa wilayani na mkoani.Hivyo ndivyo kampuni
ya Power Poll ilivyofanya”alifafanua.
Akifafanua,Kasambala
alisema wakati wa kulipa fidia walengwa wote walielimishwa taratibu na
sheria zilizofuatwa katika kufikia kila kiwango cha fidia kwa
mhusika.Wote walikubaliana na hatua hiyo na kupokea fidia kwa roho
nyeupe na kusaini kwenye daftari.Amedai fidia hiyo ililipwa katika ofisi
ya Mkuu wa wilaya.
Imeandaliwa na Nathaniel Limu, Singida
0 comments:
Post a Comment