NEWSPOINTTZ.BLOGSPOT.COM

Taarifa Ya TRA Kuhusu Tishio la wafanyabiashara kufunga maduka


Mojawapo ya wajibu wa kisheria wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ni kukagua taarifa za wafanyabiashara ili kuhakiki usahihi wa kumbukumbu za biashara. 

Katika kutekeleza zoezi hili, TRA imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwaelimisha wafanyabiashara juu ya umuhimu wa kutunza kumbukumbu za biashara na kusisitiza utumiaji wa mashine za kielektroniki za kodi (EFDs). 

Wakati wa kutekeleza jukumu hilo TRA ilibaini wafanyabiashara wengi wanakiuka sheria za kodi kwa kutokutoa risiti, hivyo wamekuwa wanachukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.

Vilevile Mamlaka ya Mapato Tanzania imebaini kuwa kuna njama ya baadhi ya wafanyabiashara kuhamasisha wenzao nchi nzima kufunga biashara kwa makusudi endapo tutaendelea na ufuatiliaji na uhakiki wa bidhaa zilizouzwa bila kutolewa risiti na kutekeleza agizo la serikali la kusitisha matumizi ya kodi elekezi kwa bidhaa zinazoingizwa nchini. Njama hizi ni ukiukwaji wa sheria na hazipaswi kuvumiliwa.

Wafanyabiashara na wananchi wote kwa ujumla wanafahamishwa kwamba kutokutoa risiti baada ya kufanya mauzo au kutoa huduma ya kibiashara ni kosa la jinai linalostahili adhabu. 

Hivyo wafanyabiashara wanatahadharishwa kutofunga maduka kutokana na sababu zinazotolewa na wafanyabiashara wanaofanya njama hizo.

Endapo TRA itawabaini wafanyabishara wanaokula njama hizi itachukua hatua kali za kisheria dhidi yao ambazo zitapelekea kuzuiwa kufanya biashara moja kwa moja hapa nchini.
 
TRA inatoa wito kwa wananchi wote kudai risiti kila wanapofanya manunuzi na kutoa taarifa za wafanyabiashara ambao hawatoi risiti. Vilevile wanaombwa kutoa taarifa katika ofisi yoyote ya TRA za kuwafichua wafanyabiashara wanaokula njama za kuhamasisha wenzao nchi nzima kufunga biashara kwa makusudi.

Taarifa hizi zinaweza kutolewa pia kupitia namba za simu zifuatazo: 0800780078 au 0800750075.

Barua pepe
Huduma@tra.go.tz
au services@tra.go.tz

Share on Google Plus

News Point inakusogezea habari kubwa za kila siku kutoka kila kona ya dunia. Ungana nasi kupitia Facebook , Twitter na Instagaram ili uwe wa kwanza kupata habari.

0 comments:

Post a Comment