Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amesema
mafisadi walioinyonya nchi katika Serikali ya awamu ya nne, ndiyo
wanaoona utawala wa Rais John Magufuli haufai.
Akizungumza masuala ya
kitaifa kwa kifupi, huku akitoa mafundisho kwa waumini wake jana katika
ibada kanisani kwake, Gwajima alimtaka Dk Magufuli aendelee kushikilia
uzi huo huo bila kuulegeza.
Gwajima ambaye mwaka jana, wakati wa
vuguvugu za kampeni ya Uchaguzi Mkuu, aliwahi kusema wasiopenda kuona
yeye akimsaidia aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward
Lowassa basi wachukue ndimu wale, jana alisema mafisadi ni wachache na
Magufuli anafanya kazi ili kuhakikisha Watanzania wengi wananufaika na
uongozi wake.
Mara kadhaa, Askofu Gwajima alikaririwa akisema kuwa atamsaidia kiongozi yeyote mwenye lengo la kuleta mabadiliko ya taifa, bila
kujali anatoka chama gani.
Katika mikutano yake, Gwajima alikuwa
akiwataka waumini wake kuchagua kiongozi wanayedhani atawaletea
mabadiliko, na alikaririwa na vyombo vya habari akiingia katika
malumbano makali na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilibrod Slaa
ambaye mbele ya waumini wake alimwita kuwa ni rafiki yake.
Jana
akimzungumzia zaidi Dk Magufuli, Askofu Gwajima alisema, “wasikukatishe
tamaa endelea hivyo hivyo kuna wanyonyaji walipenyeza mirija yao katika
Serikali iliyopita wakati wao umefika, wanatapatapa.”
Askofu Gwajima
alisema yeye ataendelea kupambana na ufisadi kumsaidia Dk Magufuli kwa
kutumia jina la Yesu Kristo na si vyombo vya dola.
Alisema mkono wake ni
mgumu kama wa chuma na kwamba kwa kulitumia jina hilo, hawezi kushindwa kuwashughulikia watu wa aina
hiyo.
“Nitatumia jukwaa hili hili la Yesu Kristo kuwasambaratisha
wasioitakia mema Serikali ya Magufuli, kwani zama zao zimekwisha,”
alisema.
Askofu huyo alisema kuna taasisi zilifikia hatua ya kutengeneza
magonjwa na hizo hizo zinatoa misaada ya dawa kwa Tanzania.
“Yaani
makampuni yanatengeneza magonjwa halafu hao hao wanatoa misaada ya
dawa hizo kwa Tanzania, unajiuliza ilikuwa serikali ya namna gani,”
alisema.
Alisema taasisi hizo ziko tayari kuua Watanzania ili kujipatia
fedha chafu ambazo maisha ya ndugu zetu yanapotea.
“Kuna watu
wananiuliza Gwajima Ufufuo na Uzima ni kanisa, dhehebu au wanaharakati
unasema kila kasoro iliyo mbele yako, nikawajibu ni majeshi ya Yesu
Kristo,” alisema.
Aliyataka madhehebu mengine ya dini kukemea maovu ili
kuleta maisha bora ya waumini wao.
Gwajima aliwataka waumini hao,
kutumia jina la Yesu Kristo kila wanafanya ibada kwani maombi yao
yatajibiwa kwa kutaja jina hilo.
chanzo>mpekuzi
0 comments:
Post a Comment