Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amezindua rasmi mbio za Mwenge wa Uhuru kwenye Uwanja wa Jamhuri Mkoani Morogoro leo.
Katika
uzinduzi huo, Makamu wa Rais alimnukuu Baba wa Taifa, Mwl Julius
Nyerere akisema kuwa nia ya Mwenge wa Uhuru tangu mwanzo ni kumulika
mipaka ya nchi yetu dhidi ya maadui, kuleta matumaini pale ambapo hakuna
matumaini, kuondoa chuki pale ambapo kuna chuki na kuleta heshima pale
ambapo kuna dharau.
Alisema
nia hiyo ya kuwepo kwa Mwenge wa Uhuru kama alivyomnukuu Baba wa Taifa,
inaendana na dhana ya kutumbua majipu katika Serikali ya awamu ya tano.
Alisema utumbuaji majipu unalenga kuleta matumaini kwa wananchi ambao
wamekata tamaa na kuleta heshima kwa wananchi waliodharauliwa.
“Kaulimbiu ya mbio ya za mwenge mwaka huu ni hii: Vijana ni nguvu kazi ya taifa, washirikishwe na wawezeshwe,”alisema
Makamu wa Rais na kuongeza kuwa vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya taifa
hawajatumika ipasavyo kutokana na sababu mbalimbali.
Alizitaja
baadhi ya sababu au changamoto zinazowakabili vijana nchini kuwa ni
ukosefu wa ajira, uwezo mdogo wa kuajiri kwenye soko la ajira, ukosefu
wa mitaji rafiki kwa vijana, maeneo ya kufanyia kazi pamoja na mitazamo
hasi kwa baadhi ya vijana kwa kuchagua kazi.
Makamu wa Rais pia amewataadharisha vijana kutokana na ongezeko kubwa la maambukizi ya ukimwi na matumizi ya madawa ya kulevya.
Amesema vijana wenye umri kati ya miaka 16-24 ndiyo wanaongoza kwa kuathiriwa na maambukizi ya ukimwi.
Amesema
athari za ukimwi na madawa ya kulevya kwa vijana ni kubwa lakini pia
zinaongeza mzigo kwa jamii na serikali katika kuwatibu, kuwahudumia na
kuongezeka kwa vifo.
Kwa
upande wake, Waziri Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama,
amemtambulisha George Jackson Kijimba kuwa ndiye kiongozi wa mbio za
mwenge mwaka huu akisaidiana na wakimbiza mwenge wengine watano.
Alisema sherehe za kuhitimisha mbio hizo za mwenge wa uhuru zitafanyika mkoani Simiyu tarehe 14 Oktoba mwaka huu.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan,
akimkabidhi Mwenge wa Uhuru kiongozi wa mbio za Mwenge kwa mwaka 2016
George Jackson Mbijima kutoka mkoa wa Mbeya kwa ajili ya kukimbiza
mwenge huo katika Mikoa na wilaya zote za Tanzania.Picha na OMR
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan,
akihutubia Taifa kwenye Sherehe za uzinduzi wa Mwenge wa Uhuru kitaifa
zilizofanyika leo april 18, 2016 katika Uwanja wa Jamhuri Mkoani
Morogoro.
0 comments:
Post a Comment