Kaimu
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Said Amanzi, amewataka wakazi wa mji wa
Singida kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa mradi Kamambe wa
uendelezaji wa mji ili uweze kubadilika muonekano na kiuchumi pia.
Mradi huo unafadhiliwa na benki ya dunia (WB) kwa gharama ya zaidi ya shilingi Bilioni 6.1.
Amanzi
ambaye ni mkuu wa wilaya ya Singida, ametoa wito huo juzi wakati
akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano wa wadau wa mpango kamambe
(master plan) wa maandalizi ya kupokea mpango ulioandaliwa kwa ajili ya
dira ya maendeleo ya mji wa Singida, kwa kipindi cha miaka 20 kuanzia
mwaka huu hadi 2036.
Alisema
uzoefu unaonyesha kuwa baadhi ya wakazi wa mji na Manispaa ya Singida
kwa ujumla, wamekuwa wakizuia bila sababu za msingi wawekezaji kuwekeza
katika maeneo ya ardhi yaliyowazi kwa madai kwamba ni mali ya ukoo wao.
“Ndugu
zangu wakazi wa mji wa Singida na manispaa kwa ujumla, nawasihi acheni
tabia ya umwinyi … msing’ang’anie ardhi ambayo hamuwezi kuiendeleza. Na
acheni misimamo hasi, misimamo ya aina hii itadumaza kabisa maendeleo ya
mji wetu,” alisema.
Kaimu
mkuu huyo wa mkoa,amewataka wawe na mitizamo chanya na pia watoe
ushirikiano wa dhati katika kutekeleza mradi wa uendelezaji wa mji wa
Singida,ili mji uweze kuvutia kwa sura na kuinua uchumi wake.
Awali
haimu mkurugenzi wa manispaa ya Singida,Deus Lusiga,alitaja baadhi ya
shughuli za mipango ya uendeshaji wa mji wa Singida, kuwa ni kusimamia
na kuongoza uendeshaji wa mji na kudhibiti ukuaji wa mji na ujenzi
holela.
“Pia
ni kupanga maeneo ya matumizi mbali mbali yakiwemo makazi, viwanda,
biashara, taasisi, miundombinu ya huduma za kijamii na maeneo ya
uwekezaji. Vile vile tunadhibiti uharibifu wa mazingira na kutangaza
fursa na vivutio vya kiutalii,” alisema Lusiga.
Aidha,
alitaja malengo makubwa ya mpango huo kamambe ni uhimizaji wa mji kuwa
pamoja na usiotawanyika, mji ulio kamilifu wenyewe na mazingira
yanayouzunguka na kuwa endelevu na kuzingatia mabadiliko ya tabia nchi.
“Nia
ya mpango huu ni kuwa na barabara na mitaa yenye ukumbwa wa kutosha kwa
ajili ya usafiri na usafirishaji, matumizi ya ardhi yaliyopangwa na
kujitosheleza na huduma zilizoboreshwa za kuiwezesha jamii kuishi
vizuri,” alifafanua.
Halmashauri
ya Singida, ni moja kati ya halmashauri 18 nchini zinazonufaika na
mradi wa uendeshaji wa miji unaofadhiliwa na benki ya dunia
(WB).Halmashauri zingine ni Babati, Geita, Bariadi, Musoma, Bukoba,
Shinyanga, Tabora, Sumbawanga, Mpanda, Songea, Moshi, Lindi, Kibaha,
Morogoro, Korongwe, Iringa na Njombe.
Na Nathaniel Limu
Ramani ya master plan ya mji wa Singida kwa kipindi cha miaka 20 kuanzia mwaka huu hadi 2036.
Bango la mkutano wa wadau wa mpango wa miaka 20 wa mji wa Singida.
Baadhi
ya wajumbe wa mkutano wa wadau wa mpango kamambe (master plan) kwa
maandalizi ya kupokea mpango ulioandaliwa kwa ajili ya dira ya maendeleo
ya mji wa Singida kwa kipindi cha miaka 20 kati ya 2016 hadi
2036.Mkutano huo ulifanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa VETA mjini
hapa.
Kaimu
Mkurugenzi Manispaa ya Singida, Deus Lusiga, akitoa taarifa yake kwenye
mkutano wa wadau wa mpango kamambe (master plan) kwa maandalizi ya
kupokea mpango ulioandaliwa kwa ajili ya dira ya maendeleo ya mji wa
Singida kwa kipindi cha miaka 20 kati ya 2016 hadi 2036.Mkutano huo
ulifanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa VETA mjini hapa.Wa pili kushoto
ni kaimu mkuu wa mkoa wa Singida, Saidi Amanzi na watatu kushoto ni
mstahiki meya manispaa ya Singida, Chima Gwae. Kushoto ni mwenyekiti wa
mkutano huo, Shaban Mwanja.
0 comments:
Post a Comment