Alhamisi August 4, mashindano ya soka la mchangani ‘Ndondo’ yalipiga hatua nyingine baada ya kutoka uswazi na kutinga katika ubalozi wa China nchini Tanzania kwa mwaliko maalum wa chakula cha jioni.
Ubalozi wa China chini ya balozi Dkt. Lu Youqing ulizialika timu tatu zilizofanya vizuri kwenye mashindano ya Sports Extra Ndondo Cup msimu huu wa 2016.
Timu zilizoalikwa kwenye chakula cha jioni kwenye ubalozi wa Chini ni pamoja na washindi wa tatu wa mashindano hayo Makumba FC, washindi wa pili Kauzu FC na mabingwa wa michuano hiyo Temeke Market.
Timu hizo ziliongonzwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mh. Paul Makonda, uwakilishi kutoka shirikisho la soka Tanzania (TFF) na uwakilishi kutoka chama cha soka mkoa wa Dar es Salaam (DRAFA).
Balozi wa China nchini Tanzania amesema, amevutiwa na mapenzi ya soka waliyonayo watanzania hasa kuanzia katika ngazi ya chini licha ya wachezaji kucheza kwenye viwanja vyenye ubora duni lakini bado wanapambana kutimiza ndoto zao.
“Mchezo wa soka ndiyo unapendwa zaidi Tanzania, katika fainali ya Ndondo Cup nimeshuhudia upendo wenu kwenye soka ingawa uwanja wa michezo si mzuri sana lakini haiathiri shauku yenu,” amesema balozi huyo ambaye aliahidi kushirikiana na serikali ya mkoa wa Dar es Salaam chini ya Mh. Paul Makonda kuboresha viwanja vya soka.
0 comments:
Post a Comment