HIKI
ndicho kipindi ambacho timu nyingi zinapambana kuwapata wachezaji ambao
zinaamini watazisaidia kwa ajili ya kupambana kwenye msimu ujao wa Ligi
Kuu Tanzania Bara.
Suala
la kusaka wachezaji wapya limekuwa na mambo mengi sana yanayojumuisha
mjadala na uamuzi wa moyo wa wachezaji husika kama wanataka kujiunga na
timu fulani au la.
Wacheaji wapya mara nyingi wanakuwa ni kipande cha kuongeza au kurekebisha kile ambacho kimekosekana katika msimu uliopita.
Kama
timu inataka kupiga hatua kutoka ilipo, au inataka kufanya vizuri zaidi
ya msimu uliopita lazima iangalie ilipokosea na inataka kufanya nini
kusonga mbele.
Mara
nyingi wakati suala hili linashughulikiwa, wadau wengi wamekuwa
wakisisitiza kwamba wachezaji wanapaswa kuwa makini sana katika suala la
uigiaji mkataba ili kuwa na uhakika na wanachokifanya kwa wakati husika
au mwafaka.
Mikataba
ni jambo muhimu kwa kuwa muunganiko wa wachezaji ana klabu wakati
mwingine unakuwa hauna tofauti na ile hadithi ya “wapendanao”. Kawaida
huanza kwa ladha tamu lakini kama kutatokea msigano, mwisho wake unakuwa
ni wenye uchachu na machungu.
Mara
nyingi, mikataba inakuwa mtetezi wa kila upande. Hivyo wanaowasisitiza
wachezaji kuwa makini na mikataba ili wasije kuchuuzwa ukifikia wakati
wa machungu, naungana nao mkono.
Lakini
pia nina ushauri tofauti, kwamba katika mikataba basi kuwe na utaalamu
wa juu wa uandikaji na klabu ziachane na kuandika mikataba ileile ya
aina ileile tokea enzi zile.
Mikataba
inaweza kugeuka msaada wa kumfanya mchezaji kukua au kubadilika.
Inavyoandikwa inaweza ikawa sehemu inayombana kuendelea kukua au
kupambana na hasa kama kweli uongozi unalenga afanye vizuri.
Mfano,
mchezaji kuwekewa kwenye mkataba wake vipengele ambavyo vinaeleza kama
wakitwaa ubingwa atapata kitu fulani kama motisha. Mfano mgawo wa kiasi
fulani kutoka katika fedha za ubingwa au vinginevyo.
,
Mchezaji
kuelezwa akiwa mfungaji bora, pamoja na kubeba kiatu na fedha kutoka
kwa wadhamini wa ligi, klabu nayo itamlipa kiasi fulani kama sehemu ya
kuonyesha kuukubali mchango wake.
Kingine
ni mchezaji kuahidiwa mfano safari na familia yake kama ataibuka
mchezaji bora mara nyingi zaidi katika kila mwezi. Mfano mchezaji bora
wa Aprili, Mei, Juni na kadhalika.
Mikataba
ya namna hiyo ndiyo imekuwa ikitumiwa na klabu kubwa kwa lengo kuongeza
hamasa ndani ya vikosi vyao kwa kuwa wanajua ushindani ni mkubwa.
Klabu
hizo ingawa zinafanya mambo mengi ni siri lakini zinajua, bado suala la
mshahara pekee haliwezi kutosha. Kumbuka soka si kazi ya kukaa ofisini,
mchezaji kila siku anapambana upya kwa maana ya kupigana kweli.
Morali
yake inapaswa kuwa juu kuanzia mazoezini na kwenye mechi. Kumbuka suala
la kuwajenga watu kisaikolojia linaweza likasaidiwa kwa kiasi kikubwa
na morali, hili ni jambo muhimu sana.
Kawaida,
klabu zimekuwa na mikataba inayofanana na ile ambayo wachezaji
waliingia na klabu hizo katika miaka ya 1990. Kuna kila sababu ya
kubadilika na kufanya mambo ambayo yataendana na hali hali au wakati
tuliopo.
Morali
ya mchezaji ni rahisi sana kuporomoka, pia ni rahisi sana kupanda hasa
kama kutakuwa na mbinu nzuri tena ndogondogo kama hizo za kuingia
mkataba wenye mkataba unaonyesha motisha lukuki na inakuwa ni zamu ya
mchezaji mwenye kuchagua azipate au la.
Kila
kitu kinabadilika kwa kasi sana katika dunia ya michezo na hasa soka.
Vizuri viongozi wa klabu wakawa wabunifu zaidi na kuangalia njia sahihi
za kupita badala ya kusimamia katika mazoea na kuona kila kitu
kinakwenda, hivyo ni poa tu.
0 comments:
Post a Comment